Sura 3

1 Wakumbushe kunyenyekea kwa watawala na wenye mamlaka, kuwatii, kuwa tayari kwa kila kazi njema. 2 kutomtusi yeyote, kutokuwa na hamu ya kupigana, na kuwa wapole, wakionyesha unyenyekevu wote kwa kila mtu. 3 Kwa maana hapo awali sisi wenyewe tulikuwa na mawazo potofu na waasi. Tulipotoshwa na kufanywa watumwa wa tamaa na anasa mbalimbali. Tuliishi katika uovu na wivu. Tulikuwa wenye kuchukiza na kuchukiana sisi kwa sisi. 4 Lakini wakati wema wa Mungu mwokozi wetu na upendo wake kwa wanadamu ulipoonekana, 5 haikuwa kwa matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa neema yake alituokoa, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa upya na kufanywa upya na Roho Mtakatifu. 6 ambaye mungu alitumiminia kwa wingi kupitia mwokozi wetu Yesu Kristo. 7 ili kwamba, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi wenye tumaini la uzima wa milele. 8 Huu ni ujumbe wa kuaminika. Ninataka usaidie katika mambo haya, ili wale waliomwamini Mungu wawe waangalifu katika jkutenda mema. Mambo haya ni mazuri na yanafaa kwa kila mtu. 9 Bali epuka mijadala ya kipumbavu na nasaba, na ugomvi, na migongano kuhusu sheria. Mambo hayo hayana faida na hayafai. 10 Mkataeni yeyote anayesababisha migawanyiko kati yenu, baada ya onyo moja ama mawili, 11 mkijua ya kuwa mtu wa namna hiyo ameiacha njia iliyo sahihi na anatenda dhambi na kujihukumu mwenyewe. 12 Nitakapomtuma kwako Artema au Tikiko, harakisha uje kwangu huku Nikopoli ambapo nimeamua kukaa kipindi cha baridi. 13 Fanya kila uwezalo kuwatuma Zena mwanasheria, na Apolo, pasipo kupungukiwa na kitu. 14 Watu wetu lazima wajifunze kujishughulisha wenyewe katika kazi nzuri zinatimiza mahitaji ya haraka, ili kwamba wasije wakawa wasiozaa matunda. 15 Wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimie wale wanaotupenda katika imani. Neema na iwe nanyi nyote.