1
Usiwe na husuda kwa wenye ubaya, wala usitamani kuambatana nao,
2
kwa sababu mioyo yao inapanga njama za vurugu na midomo yao huongea juu ya madhara.
3
Kwa hekima nyumba hujengwa na kwa ufahamu huimarishwa.
4
Kwa maarifa vyumba hujazwa vitu vyote vya thamani na utajiri wa kupendeza.
5
Shujaa wa hekima ni imara, na mtu wa maarifa huongeza nguvu zake;
6
maana kwa uongozi wa busara unaweza kufanya vita na kwa washauri wengi kuna ushindi.
7
Hekima ipo juu sana kwa mpumbavu; hafumbui kinywa chake kwenye mlango.
8
Kuna yule mwenye kupanga kufanya mabaya, watu wanamwita bwana wa njama.
9
Mipango ya mpumbavu ni dhambi na watu humchukia mwenye dhihaka.
10
Kama utakuwa dhaifu na mwenye kuogopa siku ya taabu, basi nguvu zako ni haba.
11
Waokoe wanaochukuliwa kwenda kwenye mauti na uwashikilie wale wanaopepesuka kwenda kwa mchinjaji.
12
Kama utasema, "Tazama, hatujui chochote juu ya hili," je yule anayepima mioyo hajui unachosema? Na yule anayelinda maisha yako, je hajui? Je Mungu hatampa kila mmoja kile anachostahili?
13
Mwanangu, kula asali kwa kuwa ni nzuri, kwa sababu matone ya sega la asali ni matamu unapoonja.
14
Hekima ndiyo ilivyo katika nafsi yako kama utaitafuta, tumaini lako halitabatilika na kutakuwa na tumaini.
15
Usisubiri kwa kuvizia kama waovu ambao hushambulia nyumba ya mwenye haki. Usiiharibu nyumba yake!
16
Maana mwenye haki huanguka mara saba na kuinuka tena, lakini waovu huangushwa kwa maafa.
17
Usisherekee wakati adui yako anapoanguka na wala moyo wako usifurahi anapojikwaa,
18
au Yehova ataona na kutoridhika na kuondoa ghadhabu juu yake.
19
Usifadhaike kwa sababu ya watenda mabaya, na wala usiwahusudu watu waovu,
20
maana mtu mbaya hana matumaini na taa ya watu waovu itazimika.
21
Mwanangu; mche Yehova, na umwogope mfalme, usishirikiane na watu wenye kuasi dhidi yao,
22
maana kwa ghafula msiba wao utakuja na ni nani ajuaye ukubwa wa uharibifu utakao kuja kutoka kwa hao wote?
23
Haya ni maneno ya wenye busara pia. Upendeleo katika kuhukumu kesi kwa sheria si vizuri.
24
Anayemwambia mwenye hatia, " Wewe upo sawa," atalaaniwa na watu na mataifa yatamchukia.
25
Bali wenye kuwakemea waovu watakuwa na furaha na zawadi za wema zitakuja kwao.
26
Anayetoa jibu la kweli hutoa busu kwenye midomo.
27
Andaa kazi yako ya nje, na tayarisha kila kitu kwa ajili yako mwenyewe shambani; baada ya hapo, jenga nyumba yako.
28
Usitoe ushahidi dhidi ya jirani yako bila sababu na usidanganye kwa midomo yako.
29
Usiseme, " Mimi nitamtendea kile alichonitendea; nitalipiza kwa kile alichofanya."
30
Nilikwenda jirani na shamba la mtu mvivu, nikapita kwenye shamba la mzabibu la mtu asiye na akili.
31
Miiba imeota kila sehemu, ardhi ilikuwa imefunikwa kwa upupu, na ukuta wake wa mawe ulikuwa umebomoka.
32
Kisha nikaliona na kufikiria juu yake; nikatazama na kupokea mafundisho.
33
Kulala kidogo, kusinzia kidogo, kupumzika kwa kukunja mikono kidogo
34
na umasikini huja kwa kutembea juu yako, na mahitaji yako kama askari mwenye silaha.