Wakolosai sura 2

1 Kwa kuwa nataka mfahamu jinsi ambavyo nimekuwa na taabu nyingi kwa ajili yenu,kwa wote walioko Laodikia, na kwa wote ambao hawajauona uso wangu katika mwili. 2 Nafanya kazi ili mioyo yao ifarijiwe, kwa kuletwa pamoja katika upendo na katika utajiri wote wa ufahamu kamili na maarifa, katika kuijua siri ya kweli ya Mungu, ambaye ni Kristo. 3 Katika Yeye hazina zote za hekima na maarifa zimefichwa. 4 Nasema hivi ili kwamba mtu yeyote asije akawadanganya kwa maneno ya fujo. 5 Ingawa sipo pamoja nanyi katika mwili, lakini nipo nanyi katika roho. Ninafurahi kuona utaratibu wenu mzuri na nguvu ya imani yenu katika Kristo. 6 Kama mlivyompokea Kristo Bwana, tembeeni katika yeye. 7 Mwe na mzizi ndani yake ,mjengwe juu yake, mwimarishwe katika imani kama tu mlivyofundishwa, na kufungwa katika kutoa shukrani nyingi. 8 Angalieni ya kwamba mtu yeyote asiwanase kwa falsafa na maneno matupu ya udanganyifu kwa njinsi ya mapokeo ya wanadamu, kulingana na kanuni za kidunia, na sio kwa jinsi ya Kristo. 9 Kwa maana ndani yake utimilifu wote wa Mungu unaishi katika mwili. 10 Nanyi mmejazwa katika yeye. Yeye ni kichwa juu ya kila tawala na mamlaka. 11 Katika yeye pia mlitahiriwa kwa tohara isiyofanywa na wanadamu katika kuondolewa mwili wa nyama, lakini ni katika tohara ya Kristo. 12 Mlizikwa pamoja naye katika ubatizo. Na kwa njia ya imani katika yeye mlifufuliwa kwa uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu. 13 Mlipokuwa wafu katika makosa yenu na kutokutahiriwa kwa miili yenu, aliwafanya hai pamoja naye na kutusamehe makosa yetu yote. 14 Alifuta kumbukumbu ya madeni iliyoandikwa, na taratibu zilizokuwa kinyume nasi. Aliiondoa yote na kuigongomea msalabani. 15 Aliwavunjia heshima watawala na wenye mamlaka na kuyaweka wazi kuwa sherehe ya ushidi kwa njia ya msalaba wake. 16 Kwa hiyo, mtu yeyote asiwahukumu ninyi katika kula au katika kunywa, au kuhusu siku ya sikukuu au mwezi mpya, au siku za Sabato. 17 Hivi ni vivuli vya mambo yajayo, lakini kiini ni Kristo. 18 Asiwahukumu mtu yeyote anayetaka unyenyekevu na ibada ya malaika kutokana na tuzo lako. Mtu wa jinsi hiyo huingia katika mambo aliyoyaona na kushawishiwa na mawazo yake ya kimwili. 19 Yeye hakishikilii kichwa. Ni kutoka katika kichwa kwamba mwili wote kupitia viungo vyake na mifupa huungwa na kushikamanishwa kwa pamoja; na hukua kwa ukuaji utolewao na Mungu. 20 Ikiwa mlikufa pamoja na Kristo kwa tabia za dunia, mbona mnaishi kama mnawajibika kwa dunia: 21 "Msishike, wala kuonja, wala kugusa"? 22 Vitu vyote vitaangamia kwa matumizi,sawasawa na maangizo na mafundisho ya wanadamu. 23 Sheria hizi zina hekima ya dini zilizotengenezwa kwa ubinafsi na unyenyekevu na mateso ya mwili. Lakini hazina thamani dhidi ya tamaa za mwili.