1
Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu,
2
kwa watu watatifu wa mungu na ndugu waaminifu katika Kristo walioko Kolosai. Neema iwe kwenu, na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu.
3
Tunatoa shukrani kwa Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, na tunawaombea kila mara.
4
Tumesikia imani yenu katika Yesu Kristo na upendo mlionao kwa watu wote watakatifu wa Mungu,
5
kwa sababu ya tumaini lililohifadhiwa mbinguni kwa ajili yenu, mlilolisikia kuhusu neno la ukweli, injili
6
ambayo imekuja kwenu. Na kwa njia hiyo hiyo, Injili hii inazaa tunda na inaenea ulimwenguni kote, kama vile imekuwa ikifanya kati yenu tangu siku mlipoisikia na kuielewa neema ya Mungu katika kweli.
7
Hii ndiyo injili kama mlivyojifunza kutoka kwa Epafra,mtumishi mwenzetu mpendwa aliye mtumishi mwaminifu wa Kristo kwa ajili yetu.
8
Epafra ameufanya ujulikane kwetu upendo wenu katika Roho.
9
Kwa sababu ya upendo huu, tangu siku tuliposikia hivi, hatujakoma kuwaombea.Tunawaombaea mjazwe na maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa kiroho,
10
Ili muenende kwa namna impasayo Bwana na kumpendeza katika kila namna kwa kuzaa tunda katika kila tendo jema na kukua katika maarifa ya Mungu.
11
Kwa kuimarishwa kwa nguvu zote, kwa kadiri ya uweza wa utukufu wake,ili mpate kuwa na uvumilivu na subira
12
na kumshukuru baba kwa furaha aliyewafanya ninyi mweze kuwa na sehemu katika urithi wa waumini katika nuru.
13
Naye alituokoa kutoka katika utawala wa giza, akatuhamishia katika ufalme wa Mwana wake mpendwa.
14
Ambaye ndani yake tuna ukombozi, msamaha wa dhambi.
15
Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana,mzaliwa wa kwanza wa uumbaji wote.
16
Kwa maana kwa yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyoko mbinguni na vilivyoko duniani, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana. ikiwa ni vya enzi au mamlaka au utawala au wenye nguvu, vitu vyote viliumbwa kupitia yeye na kwa ajili yake.
17
Yeye mwenyewe amekuwako kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja.
18
Na yeye ndiye kichwa cha mwili yaani kanisa, yeye ni mwanzo, na mzaliwa wa kwanza kutoka miongoni mwa wafu, hivyo, ana nafasi ya kwanza miongoni mwa vitu vyote.
19
Kwa kuwa Mungu alipendezwa kwamba utimilifu wake wote uishi ndani ya mwana.
20
na kupatanisha vitu vyote kwake kwa njia ya Mwanawe. Mungu alifanya amani kupitia damu ya msalaba wake. Akapatanisha vitu vyote kwake mwenyewe, ikiwa ni vitu vya duniani au vitu vya mbinguni.
21
Nanyi pia, kwa wakati mmoja, mlikuwa mmetengwa na Mungu na uadui katika akili na matendo maovu.
22
Lakini sasa amewapatanisha ninyi kwa mwili wake kupitia kifo ili kuwaleta ninyi watakatifu, wasio na lawama na bila dosari mbele yake,
23
kama mkiendelea katika imani, mliyoimarishwa na kuwa thabiti, pasipo kuondoshwa kutoka kwa tumaini la injili mliyoisikia. Hii ndiyo injili ambayo ilihubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu. Hii ndiyo injili ambayo kwayo mimi, Paulo, nimekuwa mtumishi.
24
Sasa nayafurahia mateso yangu kwa ajili yenu. Nami natimiliza katika mwili wangu kinachopungua kwa mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa.
25
Mimi ni mtumishi wa kanisa hili, sawasawa na wajibu niliopewa kutoka kwa Mungu kwa ajili yenu, kulitimiza neno la Mungu.
26
Hii ndiyo siri iliyofichwa tangu zamani na hata vizazi. Lakini sasa imefunuliwa kwa wote walio watakatifu wa mungu.
27
Ni kwa wale ambao Mungu alitaka kufunua ulivyo utajiri wa utukufu wa siri miongoni mwa Mataifa, ambao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu .
28
Huyu ndiye tunayemtangaza. Tunamwonya kila mtu, na kumfundisha kwa hekima yote, ili kwamba tumlete kila mtu kukomaa katika Kristo.
29
Kwa ajili hii, mimi nafanya kazi na kujitahidi kulingana na nguvu yake ifanyayo kazi ndani yangu katika uweza.