Sura 21

1 Kisha Daudi akafika Nobu kumuona Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akaja akutane na Daudi huku akitetemeka na kumwambia, "Kwa nini uko peke yako huna mtu wa kuambatana na wewe?" 2 Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, "Mfalme amenituma kwa jambo maalum na ameniambia hivi, 'Asiwepo hata mtu mmoja anayejua chochote kuhusu shughuli niliyokutuma, na kile nilichokuagiza.' Nimewaelekeza vijana kwenda sehemu fulani. 3 Sasa basi chakula gani kinapatikana hapa? Nipatie mikate mitano, au chochote kilichopo hapa." 4 Huyo Kuhani alimjibu Daudi na kusema, "Hakuna mkate wa kawaida mkononi, lakini ipo mikate takatifu- kama vijana hawajatembea na wanawake." 5 Daudi akamjibu kuhani, "Hakika hatujatembea na wanawake kwa siku hizi tatu. Nilipoanza safari, miili ya vijana iliwekwa wakfu kwa BWANA, ingawa ilikuwa safari ya kawaida. Je, si zaidi sana leo miili yao ikawekwa wakfu kwa BWANA." 6 Hivyo kuhani akampa mikate iliyokuwa imewekwa wakfu kwa BWANA. Maana haikuwepo mikate mingine hapo, isipokuwa tu ile ya wonyesho, ambayo iliondolewa kutoka kwa BWANA, ili sehemu yake iwekwe mikate ya moto, inapokuwa imeondolewa. 7 Basi siku hiyo mmoja wa watumishi wa Sauli alikuwapo mahali hapo, ameshilkiliwa mbele za BWANA. Jina la mtu huyo aliitwa Doegi Mwedomu, mkuu wa wachungaji wa Sauli. 8 Daudi akamwambia Ahimeleki, "Je, hakuna hata mkuki wowote au upanga? Maana mimi sikubeba upanga wangu wala silaha zangu, maana ile shughuli ya mfalme ilikuwa ya muhimu." 9 Kuhani akasema, "Ule upanga wa Mfilisti Goliathi, uliyemuua katika bonde la Ela, uko hapa umefunikwa katika nguo nyuma ya naivera. kama unataka kuuchukua huo, uchukue, maana hakuna silaha nyingine hapa." Daudi akasema, "Hakuna silaha nyingine kama hiyo, nipatie hiyo." 10 Daudi aliamka na kukimbia mbali na Sauli na akaenda kwa Akishi, mfalme wa Gathi. 11 Mtumishi wa Akishi akamwambia, "huyu siye Daudi mfalme wa nchi hii? Je, wanawake hawakupogezana wakiimba na kucheza, 'Sauli ameua maelfu yake, na Daudi makumi elfu yake?"' 12 Daudi akayaweka maneno hayo moyoni mwake na akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi. 13 Daudi akabadili mwenendo wake mbele yao na akajifanya kuwa mwendawazimu machoni pao; akachora-chora alama kwenye vizingiti vya milango huku akitiririsha mate yake chini ya ndevu zake. 14 Ndipo Akishi akawaambia watumishi wake, "Tazameni, mnaona mtu huyu ni mwehu. 15 Kwa nini mmemleta kwangu? Je, mimi nina haja na wehu, kumbe mmemleta mtu huyu ili anifanyie hayo mbele yangu? Hivi kweli huyu ataingia nyumbani mwangu?