1 Ilipofika siku ya Pentekoste, wote walikuwa pamoja mahali pamoja. 2 Ghafla ikatokea sauti ya mugurumo kama mvumo wa upepo mkali kutoka mbinguni, ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. 3 Hapo zikawatokea ndimi, kama za moto zimegawanyika,zikatua juu ya kila mmoja wao. 4 Wao wote wakajazwa na Roho Mtakatifu na wakaanza kusema kwa lugha zingine kama vile Roho alivyowawezesha. 5 Sasa walikuwapo wayahudi waliokuwa wanaishi Yerusalemu, wacha Mungu, kutoka kila taifa chini ya mbingu. 6 Sauti hizi ziliposikika, kundi la watu likaja pamoja wakiwa wameshanganyikiwa kwa sababu kila mtu aliwasikia wakiongea kwa lugha yake mwenyewe. 7 Waliduwaa na kushangazwa,wakasema, "Kweli, hawa wote wanaoongea siyo Wagalilaya? 8 Kwa nini sisi tunawasikia, kila mmoja kwa lugha tulizozaliwa nazo? 9 Waparthia na Wamedi na Waelamu, na hao waishio Mesopotamia, Uyahudi, na Kapadokia, na katika Ponto na Asia, 10 katika Frigia, Pamfilia, katika Misri, na sehemu ya Libya hata Kirene, na wageni kutoka Rumi, 11 Wayahudi na Waongofu, Wakrete na Waarabu, tunawasikia wakizungumza katika lugha zetu kuhusu kazi za uweza wa Mungu." 12 Wote walikuwa wameduwaa na kutatanishwa; walisemezana wao kwa wao, "Hii ina maana gani?" 13 Lakini wengine walidhihaki wakisema, "Hawa wamejazwa kwa mvinyo mpya." 14 Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti, akawaambia, "Watu wa Yudea na wote mnaoishi hapa Yerusalemu, hili lijulikane kwenu, sikilizeni kwa makini maneno yangu. 15 Watu hawa hawajalewa kama mnavyodhani, sababu saa hizi ni asubuhi saa tatu. 16 Lakini hili lilikuwa limesemwa kupitia kwa nabii Yoeli: 17 Itakuwa katika siku za mwisho; Mungu asema, nitamwaga Roho wangu kwa watu wote. Wana wenu na binti zenu watatoa unabii, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. 18 Vilevile juu ya watumishi wangu wa kiume na watumishi wangu wa kike katika siku hizo,nitamwaga Roho wangu, nao watatabiri. 19 Nitaonesha maajabu juu angani na ishara chini duniani, damu, moto, na mafusho ya moshi. 20 Jua litabadilishwa kuwa giza na mwezi kuwa damu, kabla haijaja siku kuu na ya ajabu ya Bwana. 21 Itakuwa ya kwamba kila mmoja aliitiaye jina la Bwana ataokoka. 22 Watu wa Israeli,sikieni maneno haya: Yesu wa Nazareti,mtu aliyethibitishwa na Mungu kwenu kwa matendo ya uweza na maajabu, na ishara ambazo Mungu kupitia Yeye katikati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua 23 Kwa sababu ya mpango uliokusudiwa tangu mwanzo, na maarifa ya Mungu,alitolewa nanyi, kwa mikono ya watu wahalifu,mlimsulubisha na kumuua 24 Ila Mungu alimwinua, akauondoa uchungu wa mauti kwake, kwa sababu haikuwezekana kwake kumilikiwa na kifo. 25 Hivyo Daudi anasema kuhusu yeye, 'Nilimwona Bwana daima mbele ya uso wangu, yeye yuko mkono wangu wa kulia hivyo basi sitasogezwa. 26 Kwa hiyo moyo wangu ulikuwa na furaha na ulimi wangu ulifurahishwa. Pia mwili wangu utaishi katika tumaini 27 kwa kuwa hutaiacha nafsi yangu iende kuzimu wala hutaruhusu Mtakatifu wako kuona uozo. 28 Wewe umenijulisha njia za uzima; utanifanya nijae furaha mbele ya uso wako.' 29 Ndugu,ninaweza kuzungumza kwenu kwa ujasiri kuhusu baba yetu Daudi,yeye alikufa na akazikwa, na kaburi lake liko pamoja nasi hata hivi leo. 30 Hivyo, alikuwa nabii na alijua kuwa Mungu alishaapa kwa kiapo,kwamba ataweka mmoja katika uzao wake kwenye kiti chake cha enzi. 31 Aliona yale yangetendeka baadaye kuhusu ufufuo wa Kristo, yakuwa hakuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuoza.' 32 Huyu Yesu-Mungu alimfufua, ambaye sisi wote ni mashahidi. 33 Kwa hiyo, akiwa ameinuliwa katika mkono wa kuume wa Mungu, na akiwa amepokea ahadi ya Roho Mtakatifu kutoka kwa Baba, yeye amemimina hii ahadi ambayo ninyi mnaona na kusikia. 34 Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema "Bwana alisema kwa Bwana wangu,"Keti mkono wangu wa kulia 35 mpaka nitakapowafanya adui zako kigoda kwa ajili ya miguu yako. 36 Kwa hiyo nyumba yote ya Israeli na ijue kwa hakika kwamba Mungu amemfanya Yeye kuwa Bwana na Kristo, huyu Yesu ambaye mlimsulibisha." 37 Sasa waliposikia hayo,wakachomwa katika mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, "Ndugu, tufanyeje?" 38 Na Petro akawaambia, "Tubuni na mbatizwe, kila mmoja wenu, katika jina la Yesu Kristo kwa ajili ya msamaha wa dhambi zenu, na mtapokea zawadi ya Roho Mtakatifu. 39 Kwakua ahadi ni kwenu na kwa watoto wenu na kwa wale wote walioko mbali, watu wengi kwa kadri Bwana Mungu wetu atakavyowaita." 40 Kwa maneno mengine mengi aliwashuhudia na kuwasihi,"Jiokoeni mtoke katika kizazi hiki kiovu." 41 Ndipo wakayapokea maneno yake na wakabatizwa, hapo wakaongezeka katika siku hiyo kama nafsi elfu tatu. 42 Walijitolea katika mafundisho ya mitume na ushirika,katika kuumega mkate na katika maombi. 43 Hofu ikaja juu ya kila nafsi, na maajabu mengi na ishara zikafanyika kupitia mitume. 44 Wote walioamini walikuwa pamoja na kuwa na vitu vyao kwa pamoja, 45 na waliuza vitu na milki zao na kugawanya kwa wote kulingana na mahitaji la kila mmoja. 46 Hivyo siku baada ya siku waliendelea wakiwa na lengo moja katika hekalu.Pia walimega mkate kwenye kaya, na walishiriki chakula kwa furaha na ukarimu wa mioyo, 47 wakimsifu Mungu na kuwa na kibali na watu wote,Bwana aliwaongeza siku kwa siku ambao walikuwa wakiokolewa.'