1
Kulikuwa na vita ya mda mrefu kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi. Daudi akaendelea kupata nguvu zaidi, lakini nyumba ya Sauli iliendelea kudhoofika na kudhoofika.
2
Wana wakazaliwa kwa Daudi huko Hebroni. Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni, kwa Ahinoamu wa Yezreeli.
3
Mwanawe wa pili, Kileabu, alizaliwa kwa Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli. Wa tatu, Absalomu, alikuwa mwana wa Maaka, binti Talmai, mfalme wa Geshuri.
4
Mwana wa nne wa Daudi, Adoniya, alikuwa mwana wa Hagithi. Mwanawe wa tano alikuwa Shefatia mwana wa Abitali,
5
na wa sita, Ithreamu, alikuwa mwana wa Egla mkewe Daudi. Hawa wote walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni.
6
Ikawa wakati wa vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi Abneri akajifanya mwenye nguvu katika nyumba ya Sauli.
7
Sauli alikuwa na suria jina lake Rispa, binti Aiya. Ishboshethi akamuuliza Abneri, "Kwa nini umeingia kwa suria ya baba yangu?"
8
Hata ikawa Abneri akakasirika sana kutokana na maneno ya Ishboshethi naye akasema, "Je mimi ni kichwa cha mbwa wa Yuda? Ninaonyesha uaminifu kwa nyumba ya Sauli, baba yako, kwa jamaa yake, na rafiki zake, kwa kutokukuweka katika mkono wa Daudi. Na bado leo unanishtaki kwa uovu kuhusu huyu mwanamke.
9
Mungu na anifanyie hivyo, Abneri, na kuzidi, ikiwa sitafanya kwa Daudi kama Yahwe alivyomwapia,
10
kuuhamisha ufalme kutoka nyumba ya Sauli na kukisimamisha kiti cha enzi cha Daudi juu ya Israeli na juu ya Yuda, kutoka Dani hadi Beersheba."
11
Ishboshethi hakuweza kumjibu Abneri neno tena, kwani alimuogopa.
12
Kisha Abneri akatuma wajumbe kwa Daudi kusema, "Nchi hii ni ya nani? Fanya agano nami, nawe utaona kwamba mkono wangu uko nawe, kuiIeta Israeli yote kwako."
13
Daudi akajibu, "Vema, nitafanya agano nawe. Lakini neno moja ninalolitaka kutoka kwako ni kwamba hautauona uso wangu usipomleta kwanza Mikali, binti Sauli, unapokuja kuonana nami."
14
Kisha Daudi akatuma wajumbe kwa Ishboshethi, mwana wa Sauli, kusema, "Nipe Mikali, mke wangu niliyetoa kwa ajili yake govi mia moja za Wafilisti."
15
Hivyo Ishboshethi akatuma kwa Mikali na kumchukua kutoka kwa mme wake, Paltieli mwana wa Laishi.
16
Mme wake akafuatana naye, huku akilia, akaendelea hadi Bahurimu. Kisha Abneri akamwambia, "Basi sasa rudi nyumbani." Hivyo akarudi.
17
Abneri akaongea na wazee wa Israeli kusema, "Zamani mlitaka Daudi awe mfalme wenu.
18
Basi sasa fanyeni hivyo. Kwa maana Yahwe alisema kuhusu Daudi kusema, "Kwa mkono wa Daudi mtumishi wangu nitawaokoa watu wangu Israeli kutoka katika mkono wa Wafilisti na kutoka katika mkono wa adui zao wote."
19
Pia Abneri akasema na watu wa Benjamini ana kwa ana. Kisha Abneri akaenda kuongea na Daudi huko Hebroni akaeleza kila jambo ambalo Israeli na nyumba yote ya Benjamini walitamani kulitimiza.
20
Wakati Abneri na watu ishirini kati ya watu wake walifika Hebroni kumuona Daudi, Daudi akaandaa sherehe kwa ajili yao.
21
Abneri akamueleza Daudi, "Nitainuka na kukukusanyia Israeli wote, bwana wangu mfalme, ili kwamba wafanye agano nawe, kwamba utawale juu ya yote unayotaka." Hivyo Daudi akamruhusu Abneri kuondoka, Abneri akaondoka kwa amani.
22
Kisha askari wa Daudi na Yoabu wakarudi kutoka katika kuteka nyara na wakaja na nyara nyingi. Lakini Abneri hakuwepo Hebroni pamoja na Daudi. Daudi alikuwa amemruhusu kuondoka, na alikuwa ameondoka kwa amani.
23
Wakati Yoabu na Jeshi lote walipofika, Yoabu aliambiwa, "Abneri mwana wa Neri alikuja kwa mfalme, na mfalme amemruhusu kuondoka, naye Abneri ameondoka kwa amani."
24
Kisha Yoabu akaja kwa mfalme na kusema, "Umefanya nini? Tazama, Abneri alikuja kwako! Kwa nini umemruhusu kuondoka, naye ameenda?
25
Haujui kwamba Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya na kupeleleza hali yako na kuangalia kila unalofanya?"
26
Yoabu alipoondoka kwa Daudi, alituma wajumbe kumfuatia Abneri, nao wakamrudisha kutoka katika kisima cha Sira, lakini Daudi hakulijua hili.
27
Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu alimchukua kando kati ya lango ili aongee naye faraghani. Hapohapo Yoabu alimchoma tumboni na kumuua. Hivyo, akalipa kisasi cha damu ya Asaheli nduguye.
28
Daudi alipolisikia jambo hili akasema, "Mimi na ufalme wangu hatuna hatia mbele za Yahwe daima, kuhusiana na damu ya Abneri mwana wa Neri.
29
Hatia ya damu ya Abneri na iwe juu ya Yoabu na nyumba yote ya baba yake. Na asikosekane katika familia ya Yoabu mtu mwenye vidonda, au mwenye ukoma, au kilema atembeaye kwa fimbo au aliyeuawa kwa upanga au mwenye kukosa chakula."
30
Hivyo Yoabu na Abishai nduguye wakamuua Abneri, kwa sababu alimuua Asaheli ndugu yao vitani huko Gibeoni.
31
Daudi akamwambia Yoabu na wote waliokuwa pamoja naye, "Rarueni mavazi yenu, jivikeni nguo za magunia, na muomboleze mbele ya mwili wa Abneri." Na mfalme Daudi akaufuata mwili wa Abneri wakati wa mazishi.
32
Wakamzika Abneri huko Hebroni. Mfalme akalia kwa sauti katika kaburi la Abneri, na watu wote pia wakalia.
33
Mfalme akamwomboleza Abneri naye akaimba, "Je ilipasa Abneri afe kama afavyo mpumbavu?
34
Mikono yako haikufungwa. Miguu yako haikuwa imefungwa minyororo. Kama mtu aangukavyo mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka." Watu wote wakamlilia zaidi.
35
Watu wote wakaja kumtaka Daudi ale wakati kungali mchana, lakini Daudi akaapa, "Mungu na anifanyie hivyo, na kuzidi, ikiwa nitaonja mkate au chochote kabla jua halijazama."
36
Watu wote wakaiona huzuni ya Daudi, na ikawapendeza, hivyo kila alichokifanya mfalme kikawapendeza.
37
Hivyo watu wote na Israeli yote wakatambua siku hiyo kwamba haikuwa nia ya mfalme Abneri mwana wa Neri afe.
38
Mfalme akawaambia watumishi wake, "Je hamjui kuwa mtu mkuu ameanguka leo hii katika Israeli?
39
Nami leo nimedhoofika, japokuwa nimetiwa mafuta kuwa mfalme. Watu hawa, wana wa Seruya ni hatari sana kwangu. Yahwe na amrudishie muovu kwa kumlipa kwa ajili ya uovu wake kama anavyostahili."