Sura 2

1 Ikawa baada ya haya Daudi akamuuliza Yahwe, "Je naweza kuupandia mmojawapo wa miji ya Yuda?" Yahweh akamjibu, "Panda." Daudi akauliza, "Niuendee mji upi? Yahwe akajibu, "Hebroni" 2 Hivyo Daudi akakwea pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, mjane wa Nabali. 3 Daudi akawaleta watu waliokuwa pamoja naye, na kila mmoja akaleta familia yake katika mji wa Hebroni walipoanza kuishi. 4 Kisha watu wa Yuda wakaja na kumtia Daudi mafuta kuwa mfalme juu ya nyumba ya Yuda. Wakamwambia Daudi, "Watu wa Yabeshi Gileadi wamemzika Sauli." 5 Hivyo Daudi akatuma wajumbe kwa watu wa Yabeshi Gileadi akawaambia, "Mbarikiwe na Yahwe, kwa kuwa mmeonyesha utiifu huu kwa bwana wenu Sauli mliyemzika. 6 Sasa Yahwe awadhihirishie utiifu na uaminifu wa kiagano. Nami pia nitawaonyesha wema kwa sababu ya yale mliyoyafanya. 7 Sasa basi, mikono yenu itiwe nguvu; mwe jasiri kwa maana Sauli bwana wenu amekufa, na nyumba yote ya Yuda imenitia mafuta niwe mfalme wao." 8 Lakini Abneri mwana wa Neri, mkuu wa jeshi la Sauli, akamchukuwa Ishboshethi mwana wa Sauli akamleta Mahanaimu. 9 Akamfanya Ishboshethi mfalme juu ya Gileadi, Asheri, Yezreeli, Efraimu, Benjamini na juu ya Israeli yote. 10 Ishiboshethi mwana wa Sauli alikuwa na umri wa miaka arobaini alipoanza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka miwili. Lakini nyumba ya Yuda ikaambatana na Daudi. 11 Muda ambao Daudi alikuwa mfalme juu ya nyumba ya Yuda huko Hebroni ni miaka saba na miezi sita. 12 Abneri mwana wa Neri na watumishi wa Ishboshethi mwana wa Sauli walitoka Mahanaimu kwenda Gibeoni. 13 Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wa Daudi wakatoka na kukutana nao katika bwawa la Gibeoni. Wakakaa pale, kundi moja upande huu wa bwawa na kundi lingine upande wa pili. 14 Abneri akamwambia Yoabu, "Haya, vijana na wainuke na kushindana mbele yetu." Yoabu akajibu, "Haya na wainuke." 15 Ndipo vijana walipoinuka na kukutana, kumi na wawili kwa ajili ya Banjamini na Ishboshethi mwana wa Sauli, na kumi na wawili kutoka kwa watumishi wa Daudi. 16 Kila mtu akakamata kichwa cha adui yake na kupiga upanga wake katika ubavu wa adui yake, wakaanguka chini pamoja. Kwa hiyo mahali pale pakaitwa kwa Kiebrania, "Helkath-Hasurimu," yaani "konde la upanga," lililopo Gibeoni. 17 Vita vikawa vikali sana siku ile na Abneri na watu wa Israeli wakashindwa mbele ya watumishi wa Daudi. 18 Wana watatu wa Seruya walikuwepo pale: Yoabu, Abishai na Asaheli. 19 Asaheli alikuwa mwepesi miguuni kama paa. Akamfuatilia Abneri kwa karibu bila kugeuka upande wowote. 20 Abneri akaangalia nyuma yake na kusema, "Ni wewe Asaheli?" Akajibu, "Ni mimi." 21 Abneri akamwambia, "Geuka upande wako wa kulia au kushoto umshike mmojawapo wa vijana na kuchukua silaha yake." Lakini Asaheli hakugeuka. 22 Ndipo Abneri alipomwambia tena Asaheli, "Simama usinifuate. Kwa nini nikupige hata chini? Nitautazamaje uso wa Yoabu ndugu yako?" 23 Lakini Asaheli hakukubali kugeuka; na hivyo Abneri akamchoma kwa nchi ya mkuki wake, hata ukatokea upande wa pili. Asaheli akaanguka chini akafa. Hata ikawa kila mmoja aliyefika mahali pale Asaheli alipoanguka na kufa, alisimama hapo hapo. 24 Lakini Yoabu na Abishai wakamfuatilia Abneri. Wakati jua linazama walikuwa wamefika mlima wa Amma, uliopo karibu na Gia katika njia ielekeayo nyika ya Gibeoni. 25 Wabenjamini wakajikusanya nyuma ya Abneri na kusimama juu ya kilima. 26 Kisha Abneri akamwita Yoabu na kusema, "Je! ni lazima upanga uendelee kurarua daima? Je, haujui kwamba mwisho wake utakuwa mchungu? Hata lini ndipo uwaambie watu wako waache kuwafuatia ndugu zao?" 27 Yoabu akajibu, "Kama Mungu aishivyo, usingesema hivyo, askari wangu wangewafuatia ndugu zao hata asubuhi!" 28 Ndipo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wote wakasimama na hawakuendelea kuwafuata Israeli tena wala hawakupigana tena. 29 Abneri na watu wake wakasafiri usiku wote kupitia Araba. Wakavuka Yordani, wakatembea asubuhi yote iliyofuata, na hata wakafika Mahanaimu. 30 Yoabu akarudi kutoka katika kumfuatia Abneri. Akawakusanya watu wake wote, ambopo Asahali na askari wengine kumi na tisa wa Daudi walipungua. 31 Lakini watu wa Daudi walikuwa wameua watu 360 wa Benjamini na Abneri. 32 Kisha wakamchukua Asahali na kumzika katika kaburi la baba yake, lililokuwapo Bethlehemu. Yoabu na watu wake wakasafiri usiku wote, kukacha wakati wanafika Hebroni.