1
Ndipo mke wa mmoja wa watoto wa manabii alipokuja kwa Elisha akilia, akisema, "Mtumishi wako mume wangu amekufa, na unajua kwamba mtumishi wako alikuwa anamcha BWANA. Basi aliyemdai amekuja kuwachukua watoto wangu wawili kwenda kuwa watumwa."
2
Hivyo Elisha akamwambia, "Nikusaidie nini? Niambie una nini kwenye nyumba yako?" Akamwambia "Mtumishi wako hana kitu kwenye nyumba, isipokuwa chupa ya mafuta."
3
Kisha Elisha akasema, "Nenda kaazime vyombo kwa majirani zako, vyombo vitupu. Azima vyombo vingi uwezavyo.
4
Kisha lazima uende ndani na kujifungia mlango wewe na watoto wako, na kumiminia mafuta vyombo vyote; vile vilivyojaa ukavitenge."
5
Basi akamuacha Elisha na kujifungia mlango yeye na watoto wake. Wakavileta vile vyombo kwake, na akivijaza kwa mafuta.
6
Ikawa vyombo vilipojaa, akamwambia mtoto wake, "Niletee chombo kingine." Ila akamwambia, "Hakuna vyombo vingine." Kisha mafuta yakakoma kutoka.
7
Ndipo akaja na kumwambia mtu wa Mungu. Akasema, "Nenda kauze mafuta; lipa deni lako, na yatakayobaki waachie watoto wako."
8
Siku moja Elisha alitembea Shunemu ambapo mwanamke Mwenye cheo aliishi; alimsihi ale chakula pamoja naye. Ikawa alipopita mara nyingi, angeweza kusimama pale na kula.
9
Huyo mwanamke akamwambia mme wake, "Ona, sasa nadhani kwamba huyu ni mtu mtakatifu wa Mungu ambaye hupita siku zote.
10
Ngoja tutengeneze chumba kidogo kwenye paa kwa ajili ya Elisha, na tuweke kitanda juu ya hicho chumba, meza, na taa. Kisha atakapokuwa anakuja kwetu, atakuwa anakaa hapo."
11
Ikawa siku moja akaja tena kwamba Elisha akasimama pale, akakaa kwenye hicho chumba na kupumzika hapo.
12
Elisha akamwambia Gehazi mtumishi wake, "Mwite huyu Mshunami." Wakati alipomuita, alisimama mbele yake.
13
Elisha akamwambia, "Mwambie, 'Umetusumbukia kwa kutujali. Nini kifanyike kwa ajili yako? Tunaweza kukuombea kwa mfalme au kamanda wa jeshi?'" Akajibu, "Ninaishi miongoni mwa watu wangu."
14
Kisha Elisha akajibu, "Tumfanyie nini kwa ajili yake, sasa?" Gehazi akajibu, "Kweli hana mtoto, na mume wake ni mzee."
15
Hivyo Elisha akajibu, "Mwite." Wakati alipomuita, akasimama kwenye mlango.
16
Elisha akasema, "Katika kipindi kama hiki mwakani, katika kipindi cha mwaka mmoja, utakuwa ukimkumbatia mtoto." Akasema "Hapana, bwana wangu na mtu wa Mungu, usidanganye kwa mtumishi wako."
17
Lakini yule mwanamke akabeba mimba na kujifungua mtoto wa kiume kipindi hicho hicho katika mwaka uliofuata, kama Elisha alivyokuwa amemwambia.
18
Wakati mtoto alipokuwa mkubwa, akaenda kwa baba yake siku moja, ambaye alikuwa na watu wanaovuna.
19
Akamwambia baba yake, "Kichwa changu, kichwa changu." Baba yake akamwambia mtumishi wake, "Mbebe mpeleke kwa mama yake."
20
Wakati mtumishi alipombeba kumrudisha kwa mama yake, yule mtoto alikaa kwenye magoti yake hadi mchana na baada ya hapo mtoto alikufa.
21
Hivyo yule mwanamke akambeba na kumlaza kwenye kile kitanda cha mtu wa Mungu, akafunga mlango, na kutoka nje.
22
Akamwita mume wake, na kusema, "Tafadhali nitumie mmoja wa watumishi wako na moja ya punda wako ili niweze kuwahi kwa mtu wa Mungu ili niweze kurudi."
23
Mume wake akasema, "Kwa nini unataka kwenda kwake leo? Sio mwezi mpya wala Sabato." alijibu, "Itakuwa sawa."
24
Ndipo akatandika kwenye punda na kumwambia mtumishi wake, "Mwendeshe haraka; usinipunguzie mwendo hadi nitakapokwambia ufanye hivyo."
25
Hivyo alienda na kuja na mtu wa Mungu katika mlima Karmeli. Basi wakati mtu wa Mungu alipomuona kwa mbali, akamwambia Gehazi mtumishi wake, "Tazama, mwanamke Mshunami anakuja.
26
Tafadhali mkimbilie na umwambie, 'Hamjambo kwako pamoja na mume wako na mtoto wako?'" Akajibu, "Hawajambo."
27
Baada ya kufika kwa huyo mtu wa Mungu katika mlima, alimkumbatia miguu yake. Gehazi akaja karibu ili kumuondoa lakini mtu wa Mungu akasema, "Muache, kwa kuwa amefadhaika sana. na BWANA amenificha tatizo lake kwangu, na hajaniambia kitu."
28
Ndipo akasema, "Nilikuuliza mtoto wako, bwana wangu? Sikusema, 'Usinifiche?'"
29
Ndipo Elisha akamwambia Gehazi, "Vaa kwa ajili ya safari na uchukue fimbo yangu mkononi mwako. Nenda kwake. Kama ukimkuta mtu yeyote, usimsalimie, na kama mtu yeyote akikusalimia, usimjibu. Laza fimbo yangu kwenye uso wa mtoto.
30
Lakini mama yake na huyo mtoto akasema, "Kama BWANA aishivyo, na kama uishivyo, sitakuacha." Hivyo Elisha akainuka na kumfuata.
31
Gehazi akawatangulia na kulaza ile fimbo kwenye uso wa yule mtoto, lakini yule mtoto hakuongea wala kusikia. Hivyo baada ya hapo Gehazi akarudi kuonana na Elisha na kumwambia akisema, "Mtoto hakuamka."
32
Ndipo Elisha alipofika kwenye ile nyumba, yule mtoto alikuwa amekufa na alikuwa bado yupo kwenye kitanda.
33
Hivyo Elisha aliingia ndani na kufunga mlango yeye mwenyewe na yule mtoto na kuomba kwa BWANA.
34
Alipanda juu na kulala juu ya yule mtoto; aliweka mdomo wake kwenye mdomo wake, macho yake kwenye macho yake, na mikono yake kwenye mikono yake. Akajinyoosha yeye mwenyewe kwa yule kijana, na mwili wa yule mtoto ukaanza kupata joto.
35
Baada ya hapo Elisha aliinuka na kuanza kutembea kuzunguka kile chumba na kurudi tena juu na kujinyoosha mwenyewe kwa yule kijana. Yule kijana alipiga chafya mara saba na kisha akafungua macho yake!
36
Hivyo Elisha akamwita Gehazi na kumwambia, "Mwite yule Mshunami!" Hivyo akamwita, na wakati alipofika kwenye kile chumba, Elisha akasema, "Mchukue mtoto wako."
37
Kisha akainamisha uso wake chini kwenye miguu yake na kusujudu, na kisha kumchukua mtoto wake na kuondoka.
38
Kisha Elisha akarudi tena Gilgali. Kulikuwa na njaa katika nchi, na wana wa manabii walikuwa wamekaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, "Weka sufuria kubwa kwenye moto na pika kwa ajili ya watoto wa manabii."
39
Mmoja wao akaenda kwenye shamba kukusanya mboga mboga. Alikuta matango ya porini na kukusanya ya kutosha hadi alipojaza kwenye nguo yake. Walizikata na kuziweka kwenye sufuria, lakini hakujua zilikuwa za aina gani.
40
Basi, wakawapakulia na kusambaziwa kwa watu kwa ajili ya kula. Baadaye, kadiri walivyokuwa wakiendelea kula, walipiga kelele na kusema, "Mtu wa Mungu, kuna kifo kwenye sufuria!" Hivyo wasingeweza kula tena.
41
Lakini Elisha akasema, "Lete unga." Alitupia kwenye sufuria na kusema, "Pakua kwa watu kwa ajili ya kula, kwa hiyo wanaweza kula." Kisha hapakuwa kitu chochote kibaya kwenye ile sufuria.
42
Akaja mtu kutoka Baal Shalisha kwa mtu wa Mungu na kumletea chakula cha kwanza cha mavuno yake mikate Ishirini ya shayiri, na masuke mabichi kwenye gunia. Akasema, "Wape haya watu ili waweze kula."
43
Mtumishi wake akasema, "Je, niandae hii mbele ya watu mia moja?" Lakini Elisha akasema, "Wapeni hawa watu, ili waweze kula, kwa sababu BWANA anasema, 'Watakula na kingine kitabaki."'
44
Basi mtumishi wake akawaandalia mbele yao; wakala, na kuacha kingine kimebaki, kama neno la BWANA lilivyokuwa limesema.