14
1
Mpokeeni yeyote ambaye ni dhaifu katika imani, bila kutoa hukumu kuhusu mawazo yake.
2
Mtu mmoja ana imani ya kula chochote, mwingine ambaye ni dhaifu anakula mboga tu.
3
Mtu ambaye anakula kila kitu asimdharau yeye asiyekula kila kitu. Na yeye ambaye hali kila kitu asimuhukumu mwingine ambaye hula kila kitu. Kwa kuwa Mungu amekwisha mpokea.
4
Wewe ni nani, wewe ambaye unamuhukumu mtumishi ambaye ni miliki ya mtu mwingine? Ni mbele ya Bwana wake kwamba husimama au huanguka. Lakini atainuliwa, kwa kuwa Bwana anaweza kumfanya asimame.
5
Mtu mmoja huthamini siku moja kuliko nyingine. Mwingine huthamini kila siku sawa sawa. Hebu kila mtu na ashawishike katika akili yake mwenyewe.
6
Yeye ambaye anashika siku, anashika kwa ajili ya Bwana. Na kwa yeye alaye, hula kwa ajili ya Bwana, kwa kuwa anampa Mungu shukrani. Yeye ambaye hali, hujizuia kutokula kwa ajili ya Bwana. Yeye pia hutoa shukrani kwa Mungu.
7
Kwa kuwa hakuna aishie kwa nafsi yake, na hakuna afae kwa ajili yake mwenyewe.
8
Kwa kuwa ikiwa tunaishi, tunaishi kwa ajili ya Bwana. Na ikiwa tunakufa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi ikiwa tunaishi au tunakufa tu mali ya Bwana.
9
Kwa kuwa ni kwa kusudi hili Kristo alikufa na kuishi tena, kwamba awe Bwana wa wote wafu na waishio.
10
Lakini wewe, kwa nini unamuhukumu ndugu yako? Na wewe, kwa nini unamdharau ndugu yako? Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.
11
Kwa kuwa imeandikwa, "Kama niishivyo," asema Bwana, "Kwangu mimi kila goti litapigwa, na kila ulimi utatoa sifa kwa Mungu."
12
Hivyo basi, kila mmoja wetu atatoa hesabu yake mwenyewe kwa Mungu.
13
Kwa hiyo, tusiendelee tena kuhukumiana, lakini badala yake amua hivi, kwamba hakuna atakaye weka kikwazo au mtego kwa ndugu yake.
14
Ninajua na nimeshawishika katika Bwana Yesu, kwamba hakuna kitu kilicho najisi chenyewe. Ni kwa yeye tu anayedhani kuwa chochote ni najisi, kwa kuwa kwake ni najisi.
15
Ikiwa kwa sababu ya chakula ndugu yako anahuzunika, hautembei tena katika upendo. Usimharibu kwa chakula chako mtu ambaye kwa ajili yake Kristo alikufa.
16
Hivyo msiruhusu matendo yenu mema yakasababisha watu kuwadhihaki.
17
Kwa kuwa ufalme wa Mungu si kwa ajili ya chakula na kinywaji, bali ni kwa ajili ya haki, amani, na furaha katika Roho Mtakatifu.
18
Kwa kuwa yeye amtumikiaye Kristo kwa jinsi hii amekubalika kwa Mungu na amekubalika kwa watu.
19
Kwa hiyo basi, na tufuate mambo ya amani na mambo ambayo humjenga mtu na mwingine.
20
Usiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya chakula. Vitu vyote kwa kweli ni safi, lakini ni vibaya kwa mtu yule ambaye hula na kumsababisha yeye kujikwaa.
21
Ni vyema kutokula nyama, wala kunywa divai, wala chochote ambacho kwa hicho ndugu yako hukwazwa.
22
Hizi imani maalumu ulizo nazo, ziweke kati yako mwenyewe na Mungu. Amebalikiwa yule ambaye hajihukumu mwenyewe katika kile anachokikubali.
23
Aliye na mashaka amehukumiwa ikiwa anakula, kwa sababu haitokani na imani. Na chochote kisichotokana na imani ni dhambi.