Sura 8

1 Naye Saulo alikuwa amekubali kwamba Stefano anastahili kuuawa. Siku ile ile kanisa lililokuwa katika Yerusalema lilianza kupata mateso makubwa. Waamini wote walisambaa katika Yudea na Samaria, isipokuwa mitume tu. 2 Watu wenye kuogopa Mungu wakamuzika Stefano na kumufanyia kilio kikubwa. 3 Lakini Saulo aliendelea kuteketeza kanisa, akiingia nyumba kwa nyumba, na kuwakamata waamini, wanaume na wanawake, na kwenda kuwatupa katika kifungo. 4 Wale waamini waliosambaa walikwenda popote wakitangaza Habari Njema. 5 Naye Filipo akaenda katika mji mkubwa wa Samaria na kuwahubiri wakaaji wake juu ya Kristo. 6 Makundi ya watu waliposikia maneno yale Filipo aliyosema na kuona vitambulisho alivyoonyesha, wote walimusikiliza kwa nia moja na kwa uangalifu. 7 Maana pepo walitoka ndani ya watu wengi wakilalamika kwa sauti kubwa, na watu wengi wenye kupooza pamoja na viwete waliponyeshwa vilevile. 8 Hivi kukakuwa furaha kubwa katika mji ule. 9 Na kulikuwa mtu mmoja aliyeitwa Simoni aliyekuwa akikaa katika mji ule ule tangu mbele. Yeye alikuwa akifanya mambo ya uchawi na kuwashangaza watu wa Samaria. Alijidai kuwa yeye ni mtu mkubwa. 10 Watu wote, tangia wadogo mpaka wakubwa walimusikiliza kwa uangalifu, wakisema: «Mtu huyu ndiye ule uwezo wa Mungu unaoitwa Uwezo Mkubwa.» 11 Hakika walimusikiliza vizuri kwa sababu aliwashangaza kwa muda wa siku nyingi kwa njia ya uchawi wake. 12 Lakini walipoamini Habari Njema ambayo Filipo alihubiri juu ya Ufalme wa Mungu na juu ya Yesu Kristo, wanaume na wanawake wakabatizwa. 13 Hata Simoni vilevile akaamini na kubatizwa. Na nyuma ya pale alishikamana na Filipo, naye alishangaa sana alipoona kitambulisho kikubwa na miujiza iliyokuwa ikifanyika. 14 Mitume waliokuwa Yerusalema waliposikia kwamba wakaaji wa Samaria wamekubali Neno la Mungu, wakawatumia Petro na Yoane. 15 Walipofika Samaria, wakawaombea waamini wapate kupokea Roho Mtakatifu. 16 Kwa maana Roho Mtakatifu alikuwa bado hajashuka hata juu ya mmoja wao; walikuwa tu wamebatizwa kwa jina la Bwana Yesu. 17 Halafu Petro na Yoane wakaweka mikono juu yao, nao wakapokea Roho Mtakatifu. 18 Simoni alipoona kwamba wanafunzi wamepokea Roho Mtakatifu kwa njia ya kuwekewa mikono ya mitume, akaletea Petro na Yoane feza na kuwaambia: 19 «Munipe nami vilevile uwezo huu; kusudi yeyote nitakayeweka mikono juu yake, apate kupokea Roho Mtakatifu. 20 Lakini Petro akamujibu: “Feza yako ipotelee mbali pamoja nawe, kwa sababu umezani kwamba unaweza kununua ile zawadi ya Mungu kwa njia ya feza! 21 Wewe hauna sehemu wala haki yoyote katika jambo hili, kwa sababu moyo wako si mukamilifu mbele ya Mungu. 22 Basi ugeuke toka katika zambi zako na umwombe Bwana, labda atakusamehe kwa ajili ya mawazo ya namna hii. 23 Kwa maana ninaona kwamba umejaa uchungu sana nawe umefungwa na zambi.” 24 Halafu Simoni akawaambia Petro na Yoane: “Muniombee ninyi wenyewe kwa Bwana, kusudi lisinipate hata neno moja kati ya maneno haya muliyosema.”» 25 Kisha kushuhudia na kuhubiri neno la Bwana, Petro na Yoane wakarudi Yerusalema wakitangaza Habari Njema katika vijiji vingi vya Samaria. 26 Malaika wa Bwana akamwambia Filipo: «Ujitayarishe na uende upande wa kusini kupitia njia inayotelemuka toka Yerusalema kwenda katika mji Gaza, navyo ni njia watu wasiyozoea kupitia.» 27 Basi Filipo akajitayarisha na kwenda. Alipokuwa katika njia, mara moja akakutana na towashi mmoja Mwetiopia. Mtu huyu alikuwa mkubwa, alishugulika na kazi ya usimamizi wa mali zote za malkia Kandake wa Etiopia. Yeye alikuwa amekwenda Yerusalema kwa kumwabudu Mungu, 28 na sasa alikuwa katika safari ya kurudi kwake. Alikuwa akiikaa ndani ya gari lake akisoma katika kitabu cha nabii Isaya. 29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo: «Endelea, usogee karibu na lile gari. 30 Filipo akaenda mbio karibu na gari, naye akamusikia yule mkubwa akisoma katika kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamwuliza: “Unaelewa maneno unayoyasoma?” 31 Naye akamujibu: “Nitayaelewa namna gani pasipo mtu wa kunielezea?” Halafu akamwomba Filipo apande na kuikaa karibu naye ndani ya gari. 32 Na sehemu ya Maandiko aliyokuwa akisoma ni hii: “Alipelekwa kama kondoo kwenda kuchinjwa, kama mwanakondoo anayenyamaza mbele ya mwenye kumukata manyoya. Yeye hakufungua kinywa chake. 33 Alinyenyekezwa na kuhukumiwa bila haki. Hakuna mtu atakayeweza kueleza habari za kizazi chake, maana maisha yake yameondolewa katika dunia.” 34 Yule mkubwa akamwuliza Filipo: “Ninakusihi uniambie, nabii huyu anasema juu ya nani? Ni juu yake mwenyewe au juu ya mtu mwingine?” 35 Basi Filipo akaanza na sehemu ile ile ya maandiko, akamwelezea Habari Njema juu ya Yesu. 36 Walipokuwa wakiendelea na safari, wakafika kwenye nafasi moja kwenye maji, yule mkubwa akasema: “Hapa kuna maji. Ni kitu gani kinachonizuiza nisibatizwe?”[ 37 Filipo akamwambia: “Kama unaamini kwa moyo wako wote, unaweza kubatizwa.” Yule mkubwa akamujibu: “Ninaamini kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.”»] 38 Kisha akasimamisha gari. Filipo na yule mkubwa wakashuka wote wawili ndani ya maji na Filipo akamubatiza. 39 Walipotoka ndani ya maji, kwa rafla Roho wa Bwana akamutowesha Filipo, na yule mkubwa hakumwona tena, lakini akaongeza safari yake katika furaha. 40 Filipo akajikuta amekwisha kuwa katika mji Azoto. Kisha akapita katika miji yote akihubiri Habari Njema, mpaka alipofika katika mji Kaisaria.