Sura 8

1 Katika siku hizo, kulikuwa tena na umati mkubwa, na hawakuwa na chakula. Yesu akawaita wanafunzi wake na akawaambia, 2 "Nina huruma kwa umati huu, kwa sababu wameendelea kuwa nami tayari kwa siku tatu na hawana chakula. 3 Nikiwaacha warudi majumbani mwao bila kula wanaweza wakazimia njiani kwa njaa. Na baadhi yao wametoka mbali sana." 4 Wanafunzi wake wakamjibu, "Tutaweza kupata wapi mikate ya kutosha katika sehemu kama hii isiyo na watu ili kuwashibisha watu hawa?" 5 Akawauliza, "mna mikate mingapi?" Wakasema, "Saba". 6 Akauamuru umati ukae chini. Akachukua mikate saba, akamshukuru Mungu, na kuivunja. Akawapa wanafunzi wake waiweke mbele yao, nao wakaiweka mbele ya umati. 7 Pia walikuwa na samaki wadogo wachache, na baada ya kushukuru, aliwaamuru wanafunzi wake wawagawie hivi pia. 8 Walikula na wakatosheka. Na walikusanya vipande vilivyo baki, vikapu vikubwa saba. 9 Kulikuwa na watu kama elfu nne. Kisha aliwaacha waende. 10 Mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, na wakaenda katika ukanda ya Dalmanutha. 11 Kisha Mafarisayo wakatoka na kuanza kubishana naye. Walitaka awape ishara kutoka mbinguni, ili kumjaribu. 12 Akapumua kwa kina rohoni mwake akasema, "Kwa nini kizazi hiki kinatafuta ishara? Nawaambia ninyi kweli, hakuna ishara itakayotolewa kwa kizazi hiki." 13 Kisha akawaacha, akaingia ndani ya mashua tena, akaondoka kuelekea upande mwingine. 14 Wakati huo wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate pamoja nao. Hawakuwa na zaidi ya mkate mmoja ndani ya mashua. 15 Akawaagiza akisema, "Muwe macho na mjilinde dhidi ya chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. 16 Wanafunzi walikuwa wakibishana wao kwa wao juu ya kutokuwa na mikate. 17 Yesu alipoelewa hayo, akawauiza, "Mbona mnabishana kuhusu kutokuwa na mikate? Bado hamuoni au hamuelewi? Mna mioyo migumu? 18 Mna macho, hamuoni? Mna masikio, hamsikii? Hamkumbuki? 19 Nilipoimega mikate mitano kati ya watu elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vilivyo jaa vipande vya mikate?" Wakamjibu, "kumi na mbili." 20 "Na nilipoimega mikate saba kati ya watu elfu nne, mlichukua vikapu vingapi vilivyo jaa vipande vya mikate?" Wakasema, "Saba." 21 Akawaambia, "Bado hamuelewi?" 22 Wakafika Bethsaida. Watu pale wakamlete kipofu mmoja kwa Yesu na kumsihi Yesu amguse. 23 Yesu akamshika mkono yule kipofu, na kumwongoza nje ya kijiji. Alipomtemea mate machoni na kumwekea mikono, alimuuliza, "Unaona chochote?" 24 Alitazama juu na kusema, "Naona watu wanaonekana kama miti inatembea." 25 Kisha akaweka tena mikono juu ya macho yake, na mtu yule akafungua macho yake, uwezo wake wa kuona ukarejea, naye aliona vitu vyote waziwazi. 26 Yesu akamwachilia aende nyumbani kwake na akamwambia, "Usiingie kijijini." 27 Yesu aliondoka na wanafunzi wake kwenda vijiji vya Kaiseria ya Filipi. Wakiwa njiani aliwauliza wanafunzi wake, "Watu wanasema mimi ni nani?" 28 Wakamjibu wakasema, "Yohana mbatizaji. Wengine wanasema, 'Eliya' na wengine, 'Mmoja wa Manabii." 29 Akawauliza, "Lakini ninyi mnasema mimi ni nani?" Petro akamwambia, "Wewe ni Kristo." 30 Yesu akawaonya wasimwabie mtu yeyote kumuhusu Yeye. 31 Na akaanza kuwafundisha ya kuwa Mwana wa Adamu lazima ateseke kwa mambo mengi, na atakataliwa na wazee na makuhani wakuu, na waandishi, na atauawa, na baada ya siku tatu atafufuka. 32 Aliongea ujumbe huo waziwazi. Kisha Petro akamchukua kando na akaanza kumkemea. 33 Lakini Yesu aligeuka na kuwatazama wanafunzi wake na kisha akamkemea Petro na kusema, "Nenda nyuma yangu, Shetani! Hujaweka mawazo yako kwenye mambo ya Mungu, bali ya watu." 34 Kisha akauita umati na wanafunzi wake pamoja, na kuwaambia, "Kama kuna mtu anataka kunifuata, ajikane mwenyewe, achukue msalaba wake, na anifuate. 35 Kwa kuwa yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, na yeyote atakayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya injili, atayaokoa. 36 Inamfaidia nini mtu, kuupata ulimwengu wote, na kisha kuyapoteza maisha yake? 37 Mtu anaweza kutoa nini badala ya maisha yake? 38 Yeyote anayenionea haya mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.