sura 3

1 Tena Yesu aliingia ndani ya sinagogi na palikuwa na mtu mwenye mkono uliopooza. 2 Baadhi ya watu walikuwa wakimfuatilia kwa ukaribu kuona kama atamponya siku ya Sabato ili wamshitaki. 3 Yesu alimwambia mtu mwenye mkono uliopooza, " Inuka simama katikati ya umati huu." 4 Kisha akawaambia wale watu, "Je ni halali kutenda tendo jema siku ya Sabato au kutenda yasiyo haki; kuokoa maisha, au kuua?" Lakini hawakujibu walibaki kimya. 5 Akawatazama kwa hasira, akihuzunika kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao, na akamwambia yule mtu, "Nyoosha mkono wako". Akaunyoosha na Yesu akamponya mkono wake. 6 Mafarisayo wakaenda nje wakafanya njama pamoja na herode dhidi yake ili kumuua. 7 Kisha Yesu, pamoja na wanafunzi wake, walienda baharini, na umati mkubwa wa watu uliwafuata ukitokea Galilaya na Uyahudi 8 na kutoka Yerusalemu na Idumaya na mbele ya Yorodani na Tiro na Sidoni, umati mkubwa, uliposikia kila kitu alichokuwa anakifanya, walikuja kwake. 9 Na aliwaambia wanafunzi wake kuandaa mtubwi mdongo kwa ajili yake kwa sababu ya umati, ili kwamba wasije wakamsonga. 10 Kwa kuwa aliwaponya wengi, kila mtu aliyekuwa na mateso alikuwa na shauku ya kumfikia ili amguse apone. 11 Popote roho wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kulia, na walisema, "Wewe ni Mwana wa Mungu". 12 Aliwakemea kwa msisitizo wasimfanye akajulikana. 13 Alipanda juu ya mlima, na akawaita aliowataka, na wakamwendea. 14 Akawachagua kumi na wawili (aliowaita mitume), ili kwamba wawe pamoja naye na akawatuma kuhubiri, 15 na kuwapa mamlaka ya kutoa mapepo. 16 Na akawachagua kumi na wawili: Simoni, aliyempa jina la Petro, 17 Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana ndugu yake Yakobo, aliyepewa jina la Bonagesi, hao ni, wana wa ngurumo, 18 na Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo, 19 na Yuda Iskariote, ambaye atamsaliti. 20 Kisha alienda nyumbani, na umati wa watu wakimfata kwa pamoja, tena, hata wasiweze kula mkate. 21 Familia yake waliposikia habari hiyo, walienda kumkamata, kwani walisema, " Amerukwa na akili". 22 Waandishi waliokuja kutoka Yerusalemu walisema, " Amepagawa na Beelzebuli," na, " Ni mtawala wa mapepo na anatoa mapepo". 23 Yesu aliwaita na kusema nao kwa mifano, " Jinsi gani Shetani aweza kumtoa Shetani? 24 Kama ufalme ukigawanyika wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama. 25 Kama nyumba ikigawanyika yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama. 26 Kama Shetani atainuka kinyume chake mwenyewe na kugawanyika, hawezi kusimama, atakuwa amefika mwisho wake. 27 Lakini hakuna hata mmoja awezaye kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuiba vitu vyake bila kumfunga mtu mwenye nguvu kwanza, na kisha kukusanya vilivyomo nyumbani. 28 Kweli nawambieni, dhambi zote za wana wa watu zitasamehewa, pamoja na kufuru ambazo wanatamka, 29 lakini yeyote atakaye mkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, bali ana hatia ya dhambi ya milele". 30 Yesu alilisema hili kwa sababu walikuwa wakisema, "Ana roho mchafu". 31 Kisha mama yake na ndugu zake walikuja na kusimama nje. Wakatuma mtu, kumwita. 32 Na umati wa watu uliokuwa umeketi karibu naye wakamwambia, "mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta wewe". 33 Aliwajibu, "Ni nani mama yangu na ndugu zangu?" 34 Aliwatazama waliokuwa wamekaa wamemzunguka, na akasema, "Tazama, hawa ni mama zangu na ndugu zangu! 35 Yeyote afanyaye mapenzi ya Mungu, mtu huyo ni ndugu yangu, na dada yangu, na mama yangu".