Sura 12

1 Kisha Yesu alianza kuwafundisha kwa mafumbo. Akasema, "Mtu alipanda shamba la mizabibu, akalizungushia uzio, na akachimba shimo la shinikizo la divai. Akajenga mnara na kisha akalipangisha shamba la mizabibu kwa wakulima wa mizabibu. Kisha alisafiri safari ya mbali. 2 Wakati ulipofika, alimtuma mtumishi kwa wakulima wa mizabibu kupokea kutoka kwao baadhi ya matunda ya shamba la mizabibu. 3 Lakini walimkamata, wakampiga, na wakamfukuza bila chochote. 4 Tena akatuma kwao mtumishi mwingine, na wakamjeruhi kichwani na kumtendea aibu. 5 Bado akamtuma mwingine, na huyu wakamwua. Waliwatendea wengine wengi mambo kama hayo hayo, wakiwapiga wengine na kuwaua wengine. 6 Alikuwa bado na mtu mmoja zaidi wa kutuma, mwana mpendwa. Naye akawa wa mwisho aliyetumwa kwao. Akisema, "Watamheshimu mwanangu". 7 Lakini wale wakulima wa mizabibu wakaambiana "Huyu ndiye mrithi. Njooni, tumuue yeye, na urithi utakuwa wetu." 8 Walimvamia, wakamuua na kumtupa nje ya shamba la mizabibu. 9 Kwa hiyo, Je! Atafanya nini mmiliki wa shamba la mizabibu? Atakuja na kuwaangamiza wakulima wa mizabibu na atalikabidhi shamba la mizabibu kwa wengine. 10 Hamjapata kusoma andiko hili? "Jiwe ambalo wajenzi walilikataa, limekuwa jiwe la pembeni. 11 Hili lilitoka kwa Bwana, na ni la ajabu machoni petu." 12 Baada ya haya, viongozi wa kiyahudi walitafuta njia ya kumkamata Yesu kwani walifahamu yakuwa alinena mfano huo juu yao. Lakini waliogopa umati wa watu. Hivyo walimwacha na wakaenda zao. 13 Kisha wakawatuma baadhi ya mafarisayo na maherodia kwake ili kumtega kwa maneno. 14 Walipofika, wakamwambia, "Mwalimu, kile watu wanafikiri sio wasiwasi kwako kwa sababu hauonyeshi upendeleo kwa mtu yeyote. . Unafundisha kweli njia ya Mungu. Je! Ni haki kulipa kodi kwa Kaisari au la? Je! Twaweza kulipa au la? 15 Lakini Yesu alijua unafiki wao na kuwaambia, "Kwa nini mnanijaribu? Nipeni dinari niweze kuitazama." 16 Wakaleta moja kwa Yesu. Akawaambia, "Je! ni sura na maandishi ya nani yaliyo hapa? Wakasema, "Ya Kaisari." 17 Yesu akawaambia, "Mpeni Kaisari vitu vya Kaisari na Mungu vitu vya Mungu." Wakamstaajabia. 18 Kisha Masadukayo, wasemao hakuna ufufuo, walimwendea. Wakamuwuliza, wakisema, 19 "Mwalimu, Musa alituandikia kuwa, 'Ikiwa ndugu ya mtu akifa na kumwacha mke nyuma yake, lakini hakuacha mtoto, mtu atamchukua mke wa ndugu yake, na kujipatia watoto kwa ajili ya ndugu yake.' 20 Kulikuwa na ndugu saba, wa kwanza alitwaa mke na kisha akafa, hakuacha watoto. 21 Kisha wa pili alimchukua naye akafa, hakuacha watoto. Na wa tatu hali kadhalika. 22 Na wote saba hawakuacha watoto. Mwishowe na mwanamke pia akafa. 23 Wakati wa ufufuo, watakapofufuka tena, Je! Atakuwa mke wa nani? Kwa maana ndugu wote saba walikuwa wamemwoa." 24 Yesu aliwaambia, "Je! Hii sio sababu yenu kukosea, kwa sababu hamjui maandiko wala nguvu za Mungu?" 25 Maana watakapofufuka kutoka kwa wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali ni kama malaika mbinguni. 26 Lakini, kuhusu wafu ambao wanafufuliwa, Je! Hamjasoma katika kitabu cha Musa, katika habari za kichaka, jinsi Mungu alivyosema naye na kumwambia, 'Mimi ni Mungu wa Abrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?' 27 Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Mmekosea kabisa." 28 Mmoja wa waandishi akakuja na kuyasikia mazungumzo yao; aliona kwamba Yesu aliwajibu vema. Alimwuliza, "Je! ni amri ipi iliyo ya muhimu zaidi kuliko zote?" 29 Yesu alimjibu, "Iliyo ya muhimu ni hii, "Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu, Bwana ni mmoja. 30 Lazima umpende Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa nafsi yako yote, kwa akili yako yote, na kwa nguvu zako zote.' 31 Amri ya pili ni hii, 'Lazima umpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.' Hakuna amri nyingine kuu zaidi ya hizi." 32 Mwandishi akasema, "Vema, Mwalimu! Umesema kweli kwamba Mungu ni mmoja, na kwamba hakuna mwingine zaidi yake. 33 Kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama mwenyewe, ni zaidi ya sadaka zote za kuteketezwa na dhabihu." 34 Wakati Yesu alipoona ametoa jibu la busara, akamwambia, "Wewe hauko mbali na ufalme wa Mungu." Baada ya hapo hakuna hata mmoja aliye thubutu kumwuliza Yesu maswali yoyote. 35 Na Yesu alipokuwa akifundisha hekaluni, alisema, "Je! imekuwaje waandishi husemaje kuwa Kristo ni mwana wa Daudi? 36 Daudi mwenyewe katika Roho Mtakatifu, alisema, 'Bwana alisema kwa Bwana wangu, keti katika mkono wangu wa kuume, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.' 37 Daudi mwenyewe humwita 'Bwana' Je! Kristo anaweza kua mwana wa Daudi kwa jinsi gani?" Na umati mkubwa wa watu ukamsikiliza kwa furaha. 38 Katika mafundisho yake Yesu akasema, "Jihadharini na waandishi, wanaotamani kutembea na kanzu ndefu na kusalimiwa kwenye masoko 39 na kuketi kwenye viti vya wakuu katika masunagogi na mahali pa heshima shereheni. 40 Pia wanakula nyumba za wajane na wanaomba maombi marefu ili watu wawaone. Hawa watu watapokea hukumu iliyo kuu." 41 Kisha Yesu akaketi chini karibu na sanduku la sadaka ndani ya eneo la hekalu; alikuwa akitazama watu waliokuwa wakitia pesa zao ndani ya sanduku. Watu wengi matajiri waliweka kiasi kikubwa cha pesa. 42 Kisha mwanamke mjane maskini alikuja na kutia sarafu mbili za thamani ya senti moja. 43 Akawaita wanafunzi wake na kuwaambia, "Amini nawaambia, mwanamke huyu mjane maskini ametia kiasi kikubwa zaidi ya wote ambao wameshatoa katika sanduku la sadaka. 44 Kwani wote wametoa kutokana na wingi wa mapato yao. Lakini mwanamke mjane huyu, kutoka katika umaskini wake, katia pesa yote ambayo alipaswa kuitumia kwa maisha yake."