Sura 11

1 Sasa walipokuwa wakifika Yerusalemu, walikuwa karibu na Bethfage na Bethania, kwenye Mlima wa Mizeituni, Yesu akawatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake 2 na akawaambia, "Nendeni katika kijiji kinyume na sisi. Mara mtakapoingia humo, mtamkuta mwanapunda ambaye hajapandwa. Mfungueni na mmlete kwangu. 3 Na kama yeyote akiwaambia, 'Kwa nini mnafanya hivi'?, mnapaswa kusema, 'Bwana anamhitaji na mara atamrudisha hapa'." 4 Wakaenda, wakamkuta mwana-punda amefungwa mlangoni nje ya njia kuu nao wakamfungua. 5 Na baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale wakawaambia, "Mnafanya nini, kumfungua mwana-punda huyo?" 6 Wakawaambia kama Yesu alivyowaambia, na watu wakawaacha waende. 7 Wakamleta mwana-punda kwa Yesu na wakatandika nguo zao, naye akaketi juu yake. 8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakatandaza matawi waliyoyakata mashambani. 9 Wale waliotangulia mbele yake na wale waliomfuata walipiga kelele, "Hosana! Amebarikiwa anayekuja kwa jina la Bwana. 10 Umebarikiwa ufalme ujao wa baba yetu Daudi! Hosana juu mbinguni" 11 Kisha Yesu akaingia Yerusalemu, akaingia hekaluni akatazama kila kitu. Sasa, wakati ulikuwa umeenda, alitoka kwenda Bethania pamoja nao kumi na wawili. 12 Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, aliona njaa. 13 Na akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili aone kama angeweza kupata matunda juu yake, alipofika akakuta majani tu, kwa kuwa haikuwa majira ya tini. 14 Akauambia, "Hakuna yeyote atakayekula tunda kutoka kwako tena". Na wanafunzi wake wakasikia. 15 Wafika Yerusalemu, naye akaingia hekaluni na kuanza kuwatoa nje wauzaji na wanunuzi ndani ya hekalu. Akazipindua meza za wabadilishaji wa fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 16 Hakumruhusu yeyote kubeba chochote hekaluni kilichoweza kuuzwa. 17 Akawafundisha na kusema, "Je haikuandikwa, 'nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote'? Lakini mmeifanya pango la wanyang'anyi". 18 Makuhani wakuu na waandishi walisikia alivyokuwa amesema, nao walitafuta njia ya kumwangamiza. Hata hivyo walimwogopa kwa sababu umati ulishangazwa na mafundisho yake. 19 Na jioni ilipofika, waliondoka mjini. 20 Walipokuwa wakitembea asubuhi, waliuona mti wa mtini umekauka mpaka kwenye mizizi yake. 21 Petro akakumbuka na kusema, "Rabi! Tazama, mti wa mtini ulioulaani umekauka". 22 Yesu akawajibu, "Muwe na imani katika Mungu. 23 Amini nawaambia kwamba kila auambiaye mlima huu, 'Ondoka, na ukajitupe mwenyewe baharini, 'na kama hana mashaka moyoni mwake lakini anaamini kwamba alichokisema kitatokea, hivyo ndivyo Mungu atakavyofanya. 24 Kwa hiyo ninawaambia: kila kitu muombacho na kuuliza, aminini kwamba mmepokea, navyo vitakuwa vyenu. 25 Msimamapo na kuomba, mnapaswa kusamehe chochote mlichonacho dhidi ya yeyote, ili kwamba Baba yenu aliye mbinguni awasamehe pia ninyi makosa yenu. 26 (Zingatia: Mstari huu, "Lakini msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatasamehe dhambi zenu" haumo kwenye nakala za kale). 27 Wakarudi Yerusalemu tena. Na Yesu alipokuwa akitembea hekaluni, makuhani wakuu, waandishi na wazee walikuja kwake. 28 Na wakamwambia, "Kwa mamlaka gani unafanya mambo haya?" Na ni nani aliyekupa mamlaka kuyafanya haya?" 29 Yesu akawaambia, "Nitawauliza swali moja. Niambieni na mimi nitawaambia kwa mamlaka gani ninayafanya mambo haya. 30 Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au ulitoka kwa wanadamu? Nijibuni." 31 Wakajadiliana miongoni mwao na kushindana na kusema, "Kama tukisema, 'Kutoka mbinguni,' atasema, 'Kwa nini basi hamkumwamini?' 32 Lakini kama tukisema, 'Kutoka kwa wanadamu,'..." Waliwaogopa watu, kwa kuwa wote walishawishika kwamba Yohana alikuwa Nabii. 33 Ndipo walimjibu Yesu na kusema, "Hatujui". Ndipo Yesu akawaambia, "Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani nayafanya mambo haya.