Sura 11

1 Ikawa baada ya Yesu kumaliza kuwaelekeza wanafunzi wake kumi na wawili aliondoka pale kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao, 2 Naye Yohana akiwa gerezani aliposikia habari juu ya matendo ya Kristo, alituma ujumbe kupitia wanafunzi wake, 3 na wakamuuliza, "Wewe ni yule ajaye, au kuna mwingine tunapaswa kumtazamia?" 4 Yesu akajibu na kusema kwao "Nendeni mkamwambie Yohana yale mnayoyaona na yale mnayoyasikia. 5 Watu vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wakoma wanatakaswa, watu viziwi wanasikia tena, watu waliokufa wanafufuliwa kupata uhai, na watu masikini wanahubiriwa habari njema. 6 Na amebarikiwa yule asiyeona shaka juu yangu. 7 Wakati watu hawa walipoondoka, Yesu alianza kusema na umati juu ya Yohana, "Ni nini mlikwenda kuona katika jangwa matete yakitikiswa na upepo? 8 Lakini nini mlikwenda kuona huko mtu aliyevaa mavazi mororo? Hakika, wale wavaao mavazi mororo hukaa katika nyumba za wafalme. 9 Lakini mlitoka kuona nini-Nabii? Ndiyo, nawaambia, na aliye zaidi ya Nabii. 10 Huyu ndiye aliyeandikiwa, 'Tazama, namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, ambaye ataandaa njia yako mbele yako. 11 Mimi nawaambia kweli, kati ya waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji. Lakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkubwa kuliko yeye. 12 Toka siku za Yohana Mbatizaji mpaka sasa, ufalme wa Mbinguni ni wa nguvu, na watu wenye nguvu, huuchukua kwa nguvu. 13 Kwa kuwa manabii na sheria, walikuwa wakitabiri mpaka kwa Yohana. 14 Na kama mko tayari kukubali, huyu ni Eliya, yule ajaye. 15 Aliye na masikio ya kusikia na asikie. 16 Nikifanishe na nini kizazi hiki? Ni mfano wa watoto wanaocheza maeneo ya sokoni, wanaokaa na kuitana 17 na kusema, 'Tuliwapigia filimbi na hamkucheza. Tuliomboleza, na hamukulia.' 18 Kwa kuwa Yohana alikuja bila kula mkate au kunywa mvinyo, na wakawa wanasema, 'Ana pepo.' 19 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa na wakasema 'Angalia, ni mtu mlaji na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na wenye dhambi!' Lakini hekima imejulikana kwa matendo yake.'' 20 Yesu alianza kuikemea miji ambayo baadhi ya matendo yake ya ajabu yalitendeka, kwa sababu walikuwa hawajatubu, 21 Ole wako, Kolazini, Ole wako Bethsaida! Kama matendo makuu yangefanyika Tiro na Sidoni yale yaliyofanyika hapa, wangekuwa wametubu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 22 Lakini itakuwa uvumilivu kwa Tiro na Sidoni siku ya hukumu kuliko kwako. 23 Wewe, Kapernaum, unadhani utainuliwa hadi mbinguni? Hapana utashushwa hadi chini kuzimu. Kama kwa Sodoma kungefanyika matendo makuu, kama yalifanyika kwako, ingekuwepo hadi leo. 24 Bali nasema kwako kwamba itakuwa rahisi kwa nchi ya Sodoma kusimama siku ya hukumu kuliko wewe. 25 Katika muda huo Yesu alisema, "Nakusifu wewe, Baba, Bwana wa Mbingu na Nchi, kwa sababu uliwaficha mambo haya wenye hekima na ufahamu, na kuyaweka wazi kwa wasio na elimu, kama watoto wadogo. 26 Baba kwa kuwa ilikupendeza hivyo machoni pako. 27 Mambo yote yamekabidhiwa kwangu kutoka kwa Baba. Na hakuna amjuaye Mwana isipokuwa Baba, na hakuna amjuaye Baba isipokuwa Mwana, na yeyote ambaye Mwana ana hamu ya kumfunulia. 28 Njoni kwangu, nyinyi nyote mnaosumbuka na mnaolemewa na mizigo mizito, nami nitawapumzisha. 29 Jitieni nira yangu na mjifunze kutoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mnyenyekevu na mpole wa moyo na mtapata pumziko la nafsi zenu. 30 Kwa kuwa nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.