1
Yahweh akamwambia Musa, akisema,
2
"Waamru watu wa Israeli wakuletee mafuta halisi yaliyokamliwa kutokana na mizeituni ili yatumike kwenye taa, ili kwamba taa ziweze kuwaka daima na kuleta mwanga.
3
Nje ya pazia lililoko mbele ya sanduku la maamzi ndani ya hema la kukutania, Aroni ataiwasha daima taa mbele za Yahweh, tangu asubuhi hata jioni. Hii itakuwa amri ya kudumu katika vizazi vyote vya watu wenu.
4
Kuhani mkuu atazifanya taa ziwake daima mbele za Yahweh, taa hizo zilizo kwenye kinara cha dhahabu safi.
5
Yawapasa kuchukua unga laini na kuoka kwa huo mikate kumi na miwili. Ni lazima kuwe na mbili za kumi za efa za unga katika kila mkate.
6
Kisha mtaipanga juu ya meza ya dhahabu safi mbele za Yahweh katika safu mbili, mikate sita katika kila safu,
7
Mtaweka uvumba safi kando ya kila safu ya mikata kuwa sadaka ya kuwakilisha. Uvumba huo utachomwa kwa moto kwa ajili ya Yahweh.
8
Kila siku ya Sabato kuhani mkuu sharti aipange kwa utaratibu hiyo mikate mbele za Yahweh kwa niaba ya watu wa Israeli, iwe ishara ya agano la milele.
9
Sadaka hii itakuwa kwa ajili ya Haroni na wanawe, na ni lazima waile mahali palipo patakatifu, kwa kuwa ni sehemu ya matoleo kwa Yahweh yaliyofanywa kwa moto."
10
Sasa ilitokea kwamba mwana wa mwanamke Mwisraeli, ambaye baba yake alikuwa Mmisri, alikwenda miongoni mwa watu wa Israeli. Huyu mwana wa mwanamke Mwisraeli akagombana na mwanume Mwisraeli kambini.
11
Mwana wa mwanamke Mwisraeli akalikufuru jina la Yahweh na kumlaani Mungu, kwa hiyo watu wakamleta kwa Musa. Jina la mama yake aliitwa Shelomithi, binti wa Dibri, kutoka kabila la Dani.
12
Wakamweka kizuizini mpaka Yahweh mwenyewe atakapotangaza mapenzi yake kwao.
13
Kisha Yahweh akamwambia Musa,
14
"Mchukue nje ya kambi huyo aliyemlaani Mungu. Wale wote waliomskia wataweka mikono yao juu ya kichwa chake, na kisha kusanyiko lote watamponda kwa mawe.
15
Ni lazima uwaeleze watu wa Israeli na kusema, 'Yeyote anayemlaani Mungu wake imempasa kubeba hatia yake mwenyewe.
16
Yeye anayelikufuru jina la Yahweh kwa hakika ni lazima auawe. Hakika, kusanyiko lote litampiga mawe, ama awe mgeni au Mwisraeli mwenyeji mzaliwa. Ikiwa yeyote analikufuru jina la Yahweh, ni lazima auawe.
17
Naye amuuaye mtu mwingine ni lazima kwa hakika auwe.
18
Yeye anayemuua mnyama wa mwingine sharti amfidie, uhai kwa uhai.
19
Iwapo mtu anamjeruhi jirani yake, ni lazima atendewe vivyo hivyo alivyomtendea jirani yake:
20
Mvunjiko kwa mvunjiko, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kama amesababisha jeraha kwa mtu, ndivyo ipasavyo kutendwa kwake.
21
Yeyote auaye mnyama ni lazima amfidie, na yeyote auaye mtu ni lazima auawe.
22
Ni lazima mwe na sheria moja kwa wote, mgeni na Mwisraeli mwenyeji mzaliwa, kwa kuwa Mimi ndimi Yahweh Mungu wenu."
23
Kwa hiyo Musa akazungumza na watu wa Israeli, nao watu wakamleta mwanaume huyo nje ya kambi, yule ambaye alikuwa amemlaani Yahweh. Wakampiga kwa mawe. Watu waisraeli wakaitekeleza amri ya Yahweh aliyoitoa kupitia Musa.