Sura 1

1 Unabii ambao habakuki nabii aliona. 2 '' Yahwe, kwa muda gani nitalilia msaada, na hutasikia? Nakulilia wewe , 'vurugu!' lakini hutaokoa. 3 Kwa nini unanifanya nione uovu na kuangalia matendo mabaya? Uharibifu na vurugu viko mbele yangu; kuna mapambano, na ushindani unainuka. 4 Kwa hivyo sheria ni dhaifu, na haki haidumu kwa wakati wowote. kwa kuwa waovu wanawazunguka wenye haki; kwa hivyo haki iliyopindishwa inatoweka.'' 5 "Angalia mataifa na uwachunguze; ustajaabu na ushangae! Kwa maana hakika niko karibu kufanya jambo katika siku zako ambalo hutaamini utakapoambiwa. 6 Kwa maana angalia! nakaribia kuwainua Wakaldayo _taifa katili na lenye haraka _wanapita katika upana wa nchi kuteka makao yasiyo yao. 7 Wanatisha na kuogofya; hukumu yao na ukuu wao hutoka kwao wenyewe. 8 Farasi wao pia wanambio sana kuliko chui, wakali kuliko mbwa mwitu wa jioni. Farasi wao huwaseta, na wapanda farasi wao huja kutoka mbali _ wanapaa kama tai anayewahi kula. 9 Wote huja kwa vurugu; makundi yao yanakwenda kama upepo wa jangwani, na wanakusanya mateka kama mchanga. 10 Wanawadhihaki wafalme, na watawala ni dhihaka kwao.Huicheka kila ngome, maana wanarundika udongo na kuukamata. 11 Ndipo upepo utapita; itaendelea kupita _watu wenye hatia, ambao nguvu zao ni mungu wao." 12 "Wewe si wa tangu milele, Yahwe Mungu wangu, uliye Mtakatifu wangu? Hatutakufa. Yahwe aliwatenga kwa ajili ya hukumu, nawe, Mwamba, umewaimarisha kwa ajili ya kusahihisha. 13 Macho yako ni safi mno hata yasiweze kuutazama uovu, wala huwezi kuangalia maovu kwa fadhila; kwa nini basi umeangalia kwa upendeleo ambao wanasaliti? Kwa nini unakuwa kimya wakati waovu wanawameza wenye haki kuliko wao wenyewe? 14 Unawafanya watu kama samaki baharini, kama viumbe vitambaavyo bila mtawala. 15 Huwaleta wote kwa ndoano; anawakokota watu kutoka kwenye nyavu za samaki na kuwakusanya kwenye wavu wao;kwa hiyo anashangilia na kufurahi. 16 Kwa hiyo anatoa sadaka kwa wavu wake na kuchoma ubani kwa juya lake, kwa kuwa kwa wavu wake anaishi kwa starehe,na chakula chake ni aina tajiri zaidi. 17 Kwa hiyo ataendelea kumwaga wavu wake,na kuendelea kuyachinja mataifa bila huruma?"