1
Mwanaume aliyejeruhiwa kwa kupondwa au kukatwa, haruhusiwi kuingia katika kusanyiko la Yahwe.
2
Mwana haramu haruhusiwi kuwa miongoni mwa kusanyiko la Yahwe; kutoka hadi kizazi cha kumi cha uzao wake, hakuna kati yao anatakiwa kuwa kwenye kusanyiko la Yahwe.
3
Muamori au Mmoabu haruhusiwi kuwa miongoni mwa kusanyiko la Yahwe; kutoka hadi kizazi cha kumi cha uzao wake, hakuna kati yao anatakiwa kuwa kwenye kusanyiko la Yahwe.
4
Hii ni kwa sababu hawakukutana nanyi kwa mkate na maji barabarani mlipokuwa mmetoka nje ya Misri, na kwa sababu walimkodisha Balaamu mwana wa Beoro kutoka Pethoro kule Aramu Naharaimu, awalaani.
5
Lakini Yahwe Mungu wako hakumsikiliza Balaamu; badala yake, Yahwe Mungu wako aligeuza laana kuwa baraka kwenu, kwa sababu Yahwe Mungu wako aliwapenda.
6
Hamtakiwi kutafuta amani au mafanikio yao, katika siku zenu zote.
7
Hutakiwi kumchukia Muedomi, kwa maana ni kaka yako; hutakiwi kumchukia Mmisri, kwa maana ulikuwa mgeni katika nchi yake.
8
Wazawa wa kizazi cha tatu wanaozaliwa kwao wanaweza kuwa katika kusanyiko la Yahwe.
9
Utakapotembea kijeshi dhidi ya maadui zako, basi unapaswa kujitenga na kila aina ya uovu.
10
Iwapo miongoni mwenu kuna mwanaume ambaye sio msafi kwa sababu ya jambo lililofanyika kwake usiku, basi anatakiwa atoke nje ya kambi ya jeshi; hatakiwi kurudi kambini.
11
Jioni ikifika, anatakiwa ajiogeshe kwa maji; na jua likizama atarudi ndani kambini.
12
Pia unatakiwa kuwa na eneo nje ya kambi ambayo utakwenda;
13
na utakuwa na kitu katika zana zako cha kuchimbia; utakapochuchumaa kujisaidia, unapaswa kuchimbia nacho na kisha kurudishia udongo na kufunika kile kilichotoka kwako.
14
Kwa maana Yahwe Mungu wako anatembea miongoni mwa kambi yenu kuwapa ushindi na kuwapa maadui zenu mkononi mwenu. Kwa hiyo kambi yenu lazima iwe takatifu, ili kwamba asione kitu chochote kichafu miongoni mwenu na kuwaacha.
15
Hutakiwi kumrudishia bwana mtumwa aliyetoroka kwake.
16
Mruhusu aishi pamoja nawe, katika mji wowote atakaochagua. Usimuonee.
17
Hapatakiwi kuwa na kahaba wa kidhehebu miongoni mwa mabinti wa Israeli, na wala hapatakiwi kuwa na kahaba wa kidhehebu miongoni mwa wana wa kiume wa Israeli.
18
Hautakiwi kuleta mshahara wa kahaba au mshahara wa mbwa katika nyumba ya Yahwe Mungu wako kwa kiapo chochote; kwa maana vyote hivi na machukizo mbele ya Yahwe Mungu wako.
19
Hutakiwi kumkopesha Muisraeli mwenzako kwa riba – riba ya fedha, riba ya chakula, au riba ya kitu chochote kinachokopeshwa kwa riba.
20
Kwa mgeni unaweza kukopesha kwa riba; lakini kwa Muisraeli mwenzako haupaswi kukopesha kwa riba, ili kwamba Yahwe Mungu wako aweze kukubariki katika kila jambo uwekalo mkono wako, katika nchi ambayo mnaenda kumiliki.
21
Unapofanya kiapo kwa Yahwe Mungu wako, haupaswi kukawia kuikamilsha, kwa maana Yahwe Mungu wako hakika atadai kiapo hicho; itakuwa dhambi kwako usipokamilisha.
22
Lakini iwapo utajizuia kutoa kiapo, haitakuwa dhambi kwako.
23
Kile ambacho kimetoka kinywani mwako unapaswa kukifuata na kukitekeleza; kulingana na kiapo ulichotamka kwa Yahwe Mungu wako, chochote ulichotamka kwa hiari kwa kinywa chako.
24
Utakapokwenda katika shamba la mizabibu la jirani yako, unatakiwa kula mizabibu idadi yoyote unayotaka, lakini hautakiwi kuhifadhi yoyote katika kikapu chako.
25
Utakapokwenda katika shamba la zao lililoiva la jirani yako, unaweza kuvuna kichwa cha mavuno kwa mkono wako, lakini haupaswi kutumia mundu kuvuna zao lililoiva la jirani yako.