1
Ilimpendeza Dario kuchagua juu ya ufalme magavana wa majimbo 120 ambao wangetawala juu ya ufalme wote.
2
Juu yao kulikuwa na watawala wakuu watatu, na Daniel alikuwa mmoja wao. Hawa watawala waliwekwa ili waweze kuwasimamia magavana wa majimbo, ili kwamba mfalme asipate hasara yoyote.
3
Danieli alipambanuliwa juu ya watawala wakuu na juu ya magavana wa majimbo kwasababu alikuwa na roho isiyo ya kawaida. Mfalme alikuwa akipanga kumweka juu ya ufalme wote.
4
Basi watawala wakuu wengine na magavana wa majimbo walitafuta makosa katika kazi ambazo Danieli alizifanya kwa ufalme, lakini hawakuweza kuona ufisadi au kushindwa katika majukumu yake kwasababu alikuwa mwaminifu. Hakuna kosa au uzembe uliopatikana ndani yake.
5
Kisha watu hawa wakasema, "Hatukuweza kupata sababu yoyote ya kumshitaki huyu Danieli isipokuwa tukitafuta kitu fulani dhidi yake kuhusiana na sheria za Mungu wake.'"
6
Ndipo watawala hawa na magavana walileta mpango mbele ya mfalme. Walimwambia, "Mfalme Dario, uishi milele!
7
Watawala wote wakuu wa ufalme, magavana wa mikoa, na magavana wa majimbo, washauri, na magavana wameshauriana kwa pamoja na kuamua kuwa wewe, mfalme, unapaswa kupitisha amri na kuitekeleza, ili kwamba mtu yeyote anayefanya dua kwa muungu yeyote au mtu kwa siku thelathini, isipokuwa wewe mfalme, mtu huyo lazima atupwe katika tundu la simba.
8
Sasa mfalme, litoe agizo na utie saini nyaraka ili kwamba isije ikabadilika, kama ilivyoelekezwa katika sheria za Wamedi na Waajemi, hivyo haiweze ikabatilishwa.
9
Basi, mfalme Dario alitia saini nyaraka kwa kuifanya amri kuwa zuio.
10
Danieli alipojua kuwa nyaraka imekwisha kusainiwa kuwa sheria, alienda ndani ya nyumba yake (sasa madirisha yake katika chumba cha juu yalikuwa wazi kuelekea Yerusalemu), na alipiga magoti yake, kama alivyokuwa akifanya mara tatu kwa siku, na aliomba na kushukuru mbele ya Mungu wake, kama alivyofanya hapo kabla.
11
Kisha watu hawa walikuwa wameunda hila kwa pamoja walimwona Danieli akiomba na kutafuta kibali kutoka kwa Mungu.
12
Ndipo walipomwendea mfalme na kuongea naye kuhusiana na amri yake: "Je haukuweka amri kwamba mtu yeyote atayefanya maombi kwa muungu mwingine au kwa binadamu ndani ya siku thelathini zijazo, isipokuwa kwako wewe, mfalme, lazima mtu huyo atupwe katika tundu la simba? Mfalme akajibu, "Jambo hili ni la hakika, kama ilivyoelekezwa katika sheria za Wamedi na Waajemi; ambazo haziwezi kubatilishwa."
13
Kisha wakamjibu mfalme, " Mtu yule Daniel, ambaye ni mmoja wa watu wa mateka kutoka Yuda, hakutii wewe, mfalme wala maagizo yako uliyoyasaini. Yeye humwomba Mungu wake mara tatu kwa siku."
14
Mfalme aliposikia haya, alisikitishwa sana, alitumia akili jinsi ya kumwokoa kutoka katika utawala huu. Alisumbuka sana mpaka wakati wa kuzama kwa jua akijaribu kumwokoa Danieli.
15
Kisha watu hawa waliokuwa wamepanga njama walikusanyika kwa pamoja na mfalme, na wakamwambia, "Ujue mfalme kwamba ni sheria ya Wamedi na Waajemi kwamba hakuna amri au sanamu ambayo mfalme anaipitisha yaweza kubadilishwa."
16
Ndipo mfalme alitoa agizo, na walimleta ndani Danieli, na kisha wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, "Mungu wako, ambaye unamtumikia daima, na akuokoe.''
17
Jiwe lililetwa katika mlango wa tundu, na mfalme alilitia muhuri wa pete yake mwenyewe na pamoja na muhuri wa wakuu wake ili kwamba chochote kisiweze kubadilishwa kuhusiana na Danieli.
18
Basi mfalme alienda kwenye ikulu yake na usiku ule alikuwa na mfungo. Hakuna starehe yoyote iliyoletwa mbele yake, nao usingizi ulimkimbia.
19
Kisha katika mapambazuko mfalme aliamka na kwa haraka alienda kwenye tundu la simba.
20
Na alipokaribia kwenye tundu, alimwita Danieli kwa sauti ya huzuni, akimwambia Danieli, "Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je Mungu wako ambaye wamtumkia daima, ameweza kukuokoa kutoka katika simba?"
21
Ndipo Danieli akamwambia mfalme, "Mfalme, uishi milele!
22
Mungu wangu amemtuma mjumbe wake na amevifunga vinywa vya simba, na hawajaweza kunidhuru. Kwa kuwa sikuwa na hatia yoyote mbele yake na pia mbele yako, ewe mfalme, na sijakufanyia jambo lolote la kukudhuru."
23
Basi mfalme alikuwa na furaha sana. Alitoa agizo kwamba wanatakiwa wamtoe Danieli nje ya tundu. Hivyo Danieli aliondolewa kutoka katika tundu. Hakuna dhara lolote lililoonekana kwake, kwa kuwa alikuwa amemtumainia Mungu wake.
24
Mfalme alitoa agizo, waletwe wale watu waliomshitaki Danieli na kisha akawatupa wao katika tundu la simba--wao, na watoto wao, na wake zao. Kabla hawajafika sakafuni, simba waliwararua na kuvunjavunja mifupa yao vipande vipande.
25
Kisha mfalme Dario aliandika ujumbe kwa watu wote, mataifa na lugha ambazo ziliishi katika dunia yote: "Amani na iongezeke kwenu.
26
Ninaagiza kwamba katika utawala wote wa ufalme wangu watu watetemeke mbele ya Mungu wa Danieli na kumcha, kwa kuwa ni Mungu aliye hai na huishi milele, na ufalme wake hauwezi kuharibiwa; utawala wake utakuwepo hadi mwisho.
27
Yeye anatuhifadhi salama na kutuokoa, na anafanya ishara na maajabu mbinguni na duniani; amemhifadhi Danieli salama dhidi ya uwezo wa simba."
28
Na hivyo basi, Danieli alifanikiwa katika utawala wa Dario na katika utawala wa Koreshi Mwajemi.