1
Ikawa baada ya haya Absalomu akaandaa gari la farasi na farasi kwa ajili yake pamoja na watu hamsini wa kwenda mbele zake.
2
Absalomu alikuwa akiamka mapema na kusimama kando ya njia iliyoelekea katika lango la mji. Mtu yeyote aliyekuwa na shauri la kuja kwa mfalme kwa ajili ya hukumu, Absalomu alimwita na kumuuliza, "Unatoka mji upi?" Na mtu yule hujibu, Mtumishi wako anatoka mojawapo ya kabila za Israeli."
3
Hivyo Absalomu angemwambia, "Tazama, shitaka lako ni jema na la haki, lakini hakuna aliyepewa mamlaka na mfalme kusikiliza shitaka lako.
4
Absalomu uongeza, "Natamani kwamba ningefanywa mwamuzi ndani ya nchi ili kwamba kila mtu aliye na shitaka angeweza kuja kwangu nami ningempa haki.
5
Hivyo ikawa kila mtu aliyekuja kumheshimu Absalomu yeye angenyosha mkono na kumshika na kumbusu.
6
Absalomu alifanya hivi kwa Israeli wote waliokuja kwa mfalme kwa ajili ya hukumu. Hivyo Absalomu akaipotosha mioyo ya watu wa Israeli.
7
Ikawa mwishoni mwa miaka minne Absalomu akamwambia mfalme, "Tafadhali niruhusu niende ili nitimize nadhili niliyoiweka kwa Yahwe huko Hebroni.
8
Kwa maana mtumishi wako aliweka nadhili alipokuwako Geshuri katika Shamu akisema, 'Ikiwa Yahwe kweli atanirejesha Yerusalemu, ndipo nitamwabudu yeye."
9
Hivyo mfalme akamwambia, "Nenda kwa amani". Absalomu akainuka na kwenda Hebroni.
10
Kisha Absalomu akatuma wapelelezi katika jamaa zote za Israeli, kusema, "Mara msikiapo sauti ya tarumbeta semeni, 'Absalomu anatawala katika Hebroni."
11
Watu mia mbili waliokuwa wamealikwa kutoka Yerusalemu wakaenda na Absalomu. Wakaenda katika ujinga wao bila kujua Absalomu alichokipanga.
12
Wakati Absalomu akitoa dhabihu, alituma watu kwa Ahithofeli katika mji wake huko Gilo. Yeye alikuwa mshauri wa Daudi. Fitina za Absalomu zikawa na nguvu kwa kuwa watu waliomfuata waliendelea kuongezeka.
13
Mjumbe akaja kwa Daudi na kusema, "Mioyo ya watu wa Israeli inaambatana na Absalomu."
14
Hivyo Daudi akawaambia watumishi wake waliokuwa pamoja naye huko Yerusalemu, "Haya na tuinuke na kukimbia kwani hakuna hata mmoja atakayeokoka kwa Absalomu. Jiandaeni kuondoka mara moja asije akatupata mara hata akasababisha madhara juu yetu na kuushambulia mji kwa makali ya upanga."
15
Watumishi wa mfalme wakamwambia, "Tazama, watumishi wako wapo tiyari kufanya lolote bwana wetu mfalme atakaloamua.
16
Mfalme akaondoka na familia yake yote pamoja naye, lakini mfalme akawaacha wanawake kumi waliokuwa masuria wa mfalme ili walitunze kasri.
17
Baada ya mfalme kwenda na watu wote pamoja naye, wakasimama katika nyumba ya mwisho.
18
Watumishi wako wote wakaenda pamoja naye na mbele yake wakaenda Wakerethi na Wapelethi, na Wagiti mia sita wote waliokuwa wamemfuata kutoka Gathi.
19
Kisha mfalme akamwambia Itai Mgiti, "Kwa nini wewe pia uende nasi? Rudi na ukae na mfalme Absalomu kwa kuwa wewe ni mgeni tena mfungwa. Rudi mahali pako mwenyewe.
20
Kwani ni jana tu umeondoka, kwa nini nikufanye uzunguke nasi popote? Hata sijui niendako. Hivyo rudi pamoja na wenzako. Utiifu na uaminifu viambatane nawe."
21
Lakini Itai akamjibu mfalme na kusema, "Kama Yahwe aishivyo na kama bwana wangu mfalme aishivyo, kwa hakika mahali popote bwana wangu mfalme aendako, mtumishi wako pia ndipo atakapokwenda, kwamba ni maisha au kifo."
22
Hivyo Daudi akamwambia Itai, haya tangulia uende pamoja nasi." Hivyo Itai Mgiti akaenda pamoja na mfalme, pamoja na watu wake wote na familia zao zote.
23
Nchi yote ikalia kwa sauti kama watu walivyokuwa wakivuka Bonde la Kidroni, na pia mfalme naye akivuka. Watu wote wakasafiri kuelekea nyikani.
24
Walikuwepo pia Sadoki pamoja na Walawi wote wamebeba sanduku la Mungu la agano. Wakaliweka sanduku la Mungu chini na kisha Abiathari akaungana nao. Wakasubiri mpaka watu wote wakapita kutoka mjini.
25
Mfalme akamwambia Sadoki, "Ulirudishe sanduku la Mungu mjini. Ikiwa nitaona neema machoni pa Yahwe atanirudisha na kunionyesha tena sanduku na mahali likaapo.
26
Lakini ikiwa atasema, sipendezwi nawe,' tazama mimi nipo hapa, na anitendee yaliyo mema machoni pake."
27
Pia mfalme akamwambia Sadoki kuhani, "Je wewe siyo mwonaji? Rudi mjini kwa amani na wanao wawili, Ahimaazi mwanao na Yonathani mwana wa Abiathari.
28
Tazama nitasubiri katika vivuko vya nyikani mpaka nitakapo pata neno kutoka kwenu kunipasha habari."
29
Hivyo Sadoki na Abiathari wakalirudisha sanduku la Mungu Yerusalemu nao wakakaa humo.
30
Lakini Daudi akaenda bila viatu huku akilia hata Mlima wa Mizeituni, naye alikuwa amefunika kichwa chake. Kila mtu miongoni mwao waliokuwa pamoja naye akafunika kichwa chake, nao wakaenda huku wakilia.
31
Mtu mmoja akamwambia Daudi akisema, Ahithofeli ni miongoni mwa wafitini walio pamoja na Absalomu." Hivyo Daudi akaomba, "Ee Yahwe, tafadhali badili ushauri wa Ahithofeli kuwa upumbavu."
32
Ikawa Daudi alipofika juu njiani mahala Mungu alipokuwa akiabudiwa, Hushai Mwarki akaja kumlaki vazi lake likiwa limeraruliwa na mavumbi kichwani pake.
33
Daudi akamwambia, "Ikiwa utaenda nami utakuwa mzigo kwangu.
34
Lakini ukirudi mjini na kumwambia Absalomu, 'Nitakuwa mtumishi wa mfalme kama nilivyokuwa mtumishi wa baba yako, ndivyo nitakavyokuwa mtumishi wako,' ndipo utayageuza mashauri ya Ahithofeli kwa ajili yangu.
35
Je haunao pamoja nawe Sadoki na Abiathari makuhani? Hivyo chochote ukisikiacho katika kasri, uwaambie Sadoki na Abiathari makuhani.
36
Tazama wanao pamoja nao wana wao wawili, Ahimaasi, mwana wa Sadoki, na Yonathani mwana wa Abiathari. Mniletee habari juu ya kila mnachokisikia."
37
Hivyo Hushai, rafiki wa Daudi, akaja mjini wakati Absalomu anafika na kuingia Yerusalemu.