1
Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu, kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, na kwa waumini wote walioko katika mkoa wote wa Akaya.
2
Neema na iwe kwenu na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
3
Na asifiwe Mungu na Baba wa Bwana Yesu Kristo. Yeye ni Baba wa rehema na Mungu wa faraja yote.
4
Mungu hutufariji sisi katika mateso yetu yote, ili kwamba tuweze kuwafariji wale walio katika mateso. Tunawafariji wengine kwa faraja ileile ambayo Mungu alitumia kutufarij na sisi.
5
Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo huongezeka kwa ajili yetu, vile vile faraja yetu huongezeka kupitia Kristo.
6
Lakini kama tunataabishwa, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu. Na kama tunafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu. Faraja yenu inafanya kazi kikamilifu mnaposhiriki mateso kwa uvumilivu kama sisi pia tunavyoteseka.
7
Na ujasiri wetu juu yenu ni thabiti. Tunajua kwamba kama vile ambavyo mnashiriki mateso, vile vile mnashiriki faraja.
8
Kwa kuwa hatutaki ninyi muwe wajinga, ndugu, kuhusu matatizo tuliyokuwa nayo huko Asia. Tulionewa zaidi ya vile tuwezavyo kubeba, kana kwamba hatukuwa hata na tumaini la kuishi tena.
9
Kweli, tulikuwa na hukumu ya kifo juu yetu. Lakini hiyo ilikuwa ni kutufanya sisi tusiweke tumaini juu yetu wenyewe, badala yake tuweke tumaini katika Mungu, afufuaye wafu.
10
Alituokoa sisi kutoka hayo maafa ya mauti, na atatuokoa tena. Tumeweka ujasiri wetu katika yeye ya kwamba atatuokoa tena.
11
Atafanya hivi kama vile ninyi pia mtusaidiavyo kwa maombi yenu. Hivyo wengi watatoa shukurani kwa niaba yetu kwa ajili ya upendeleo wa neema tuliyopewa sisi kupitia maombi ya wengi.
12
Tunajivunia hili: ushuhuda wa dhamiri yetu. Kwa kuwa ni katika nia safi na usafi wa Mungu kwamba tulienenda wenyewe katika dunia. Tumefanya hivi hasa na ninyi, na sio katika hekima ya ulimwengu, lakini badala yake ni katika neema ya Mungu.
13
Hatuwaandikii chochote ambacho hamwezi kukisoma au kuelewa. Ninaujasiri
14
kwamba kwa sehemu mumekwisha kutuelewa. Na ninaujasiri kwamba katika siku ya Bwana Yesu tutakuwa sababu yenu kwa ajili ya kiburi chenu, kama vile mtakavyokuwa kwetu.
15
Kwa sababu nilikuwa na ujasiri kuhusu hili, nilitaka kuja kwenu kwanza, ili kwamba muweze kupokea faida ya kutembelewa mara mbili.
16
Nilikuwa napanga kuwatembelea nnyi wakati nikielekea Makedonia. Tena nilitaka kuwatembelea tena wakati nikirudi kutoka Makedonia, na kisha ninyi kunituma mimi wakati nikielekea Uyahudi.
17
Nilipokuwa nafikiria namna hii, je, nilikuwa nasitasita? Je ninapanga mambo kulingana na viwango vya kibinadamu, ili kwamba niseme "Ndiyo, ndiyo" na "Hapana, hapana" kwa wakati mmoja?
18
Lakini kama vile Mungu alivyo mwaminifu, hatusemi vyote "Ndiyo" na "Hapana."
19
Kwa kuwa mwana wa Mungu, Yesu Kristo, ambaye Silvano, Timotheo na mimi tulimtangaza miongoni mwenu, siyo "Ndiyo" na "Hapana." Badala yake, yeye wakati wote ni "Ndiyo."
20
Kwa kuwa ahadi zote za Mungu ni "Ndiyo" katika yeye. Hivyo pia kupitia yeye tunasema "Amina" kwa utukufu wa Mungu.
21
Sasa ni Mungu ambaye hututhibitisha sisi pamoja nanyi katika Kristo, na alitutuma sisi.
22
Aliweka muhuri juu yetu na alitupa Roho katika mioyo yetu kama dhamana ya kile ambacho angetupatia baadaye.
23
Badala yake, namsihi Mungu kunishuhudia mimi kwamba sababu iliyonifanya nisije Korintho ni kwamba nisiwalemee ninyi.
24
Hii sio kwa sababu tunajaribu kudhibiti jinsi imani yenu inavyotakiwa kuwa. Badala yake, tunafanya pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu, kama mnavyosimama katika imani yenu.