1
Wapendwa, msiiamini kila roho, lakini zijaribuni roho muone kama zinatokana na Mungu, kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea duniani.
2
Kwa hili mtamjua Roho wa Mungu - kila roho itakayokiri kuwa Yesu Kristo amekuja katika mwili ni wakutoka kwa Mungu,
3
na kila roho isiyomkiri Yesu si ya Mungu. Hii ni roho ya mpinga kristo, ambayo mliyoisikia kuwa inakuja, na sasa tayari iko duniani.
4
Ninyi ni wa Mungu, watoto na mmekwisha washinda kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu.
5
Wao ni wa ulimwengu, kwa hiyo wanachokisema ni cha ulimwengu, na ulimwengu unawasikiliza.
6
Sisi ni wa Mungu. Yeye amjuaye Mungu hutusikiliza sisi. Yeye asiye wa Mungu hawezi kutusikiliza. Katika hili tunajua roho wa kweli na roho wa uongo.
7
Wapendwa, tupendane sisi kwa sisi, kwa vile upendo hutoka kwa Mungu, na kila mmoja apendaye amezaliwa na Mungu na kumjua Mungu.
8
Mtu asiyependa hamjui Mungu, kwa sababu Mungu ni upendo.
9
Katika hili pendo la Mungu lilifunuliwa miongoni mwetu, kwamba Mungu alimtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni ili tuishi kupitia yeye.
10
Katika hili pendo, si kwamba tulimpenda Mungu, lakini yeye alitupenda, na akamtuma Mwanawe awe fidia kwa ajili ya dhambi zetu.
11
Wapendwa, ikiwa Mungu alitupenda sisi, vile vile tunapaswa kupendana sisi kwa sisi.
12
Hakuna hata mmoja aliyemuona Mungu. Kama tukipendana sisi kwa sisi, Mungu anakaa ndani yetu na upendo wake umekamilika ndani yetu.
13
Katika hili tunajua kuwa tunakaa ndani yake na yeye ndani yetu, kwa sababu ametupa Roho wake.
14
Tena, sisi tumeonana na kushuhudia kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa mwokozi wa ulimwengu.
15
Kila anayekiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu anakaa ndani yake na yeye ndani ya Mungu.
16
Tena tumejua na kuamini upendo alio nao Mungu kwa ajili yetu. Mungu ni pendo, na yeye anayekaa ndani ya upendo anakaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.
17
Kwa sababu hii, upendo huu umekwisha kukamilika katikati yetu, ili tuwe na ujasiri siku ya hukumu, kwa sababu kama yeye alivyo, na sisi ndivyo tulivyo katika ulimwenngu huu.
18
Hakuna hofu ndani ya pendo. Lakini pendo kamili huitupa hofu nje, kwa sababu hofu huhusiana na hukumu. Lakini yeye aogopaye hajakamilishwa katika pendo.
19
Tunapenda kwa sababu Mungu alitupenda kwanza.
20
Ikiwa mmoja atasema, "Nampenda Mungu" lakini hawezi kumpenda ndugu yake, ni mwongo. Kwa sababu asiyempenda ndugu yake, anayemuona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hajamuona.
21
Na hii ndiyo amri tuliyo nayo kutoka kwake: Yeyote ampendaye Mungu, anapaswa kumpenda ndugu yake pia.