Sura 20

1 Kisha niliona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa na ufunguo wa shimo lisilo na mwisho na mnyororo mkubwa mkononi mwake. 2 Alimshika yule joka, nyoka wa zamani, ambaye ni ibilisi au Shetani, na kumfunga miaka elfu. 3 Alimtupa kwenye shimo lisilo na mwisho, akalifunga na kulitia mhuri juu yake. Hii ilikuwa hivyo ili kwamba asiwadanganye mataifa tena mpaka miaka elfu itakapoisha. Baada ya hapo, ataachiwa huru kwa muda mchache. 4 Kisha niliona viti vya enzi. Waliokuwa wamevikalia ni wale ambao walikuwa wamepewa mamlaka ya kuhukumu. Vilevile niliona nafsi za wale ambao walikuwa wamekatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda kuhusu Yesu na kwa neno la Mungu. Walikuwa hawajamwabudu mnyama au sanamu yake, na walikataa kupokea alama juu ya paji za nyuso zao au mkono. Walirudi uhai na wakatawala pamoja na Kristo kwa miaka elfu. 5 Wafu waliobaki hawakurudi uhai mpaka miaka elfu ilipokuwa imeisha. Huu ndio ufufuo wa kwanza. 6 Mbarikiwa na mtakatifu ni mtu yeyote ambaye atashiriki katika ufufuo wa kwanza! Mauti ya pili haina nguvu juu ya watu kama hawa. Watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo na watatawala na yeye kwa miaka elfu. 7 Wakati miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa kutoka gerezani mwake. 8 Atakwenda kuwadanganya mataifa katika kona nne za dunia -Gogu na Magogu - kuwaleta pamoja kwa ajili ya vita. Watakuwa wengi kama mchanga wa bahari. 9 Walikwea juu kwenye tambarare ya nchi nao walizunguka kambi ya waumini, mji upendwao. Lakini moto ulishuka kutoka mbinguni na kuwaangamiza. 10 Shetani, ambaye aliwadanganya, alitupwa ndani ya ziwa liwakalo kiberiti, ambamo mnyama na nabii wa uongo walikuwa wameshatupwa. Watateswa mchana na usiku milele na milele. 11 Kisha niliona kiti cha enzi kikubwa cheupe na yule ambaye alikaa juu yake. Dunia na mbingu zilikimbia mbali kutoka katika uwepo wake, lakini hapakuwako nafasi ya wao kutolokea. 12 Niliwaona waliokufa - hodari na wasio wa muhimu wamesimama mbele ya kiti cha enzi, na vitabu vilifunuliwa. Kisha kitabu kingine kilifunguliwa - Kitabu cha Uzima. Wafu walihukumiwa kwa kile kilichoandikwa ndani ya vitabu, matokeo ya kile walichokifanya. 13 Bahari iliwatoa wafu ambao walikuwa ndani yake. Kifo na kuzimu viliwatoa wafu ambao walikuwa ndani yake, na wafu walihukumiwa kulingana na matendo yao. 14 Kifo na kuzimu zilitupwa ndani ya ziwa la moto. Hii ni mauti ya pili - ziwa la moto. 15 Kama jina la yeyote halikupatikana limeandikwa ndani ya Kitabu cha Uzima, alitupwa ndani ya ziwa la moto.*