Sura 42

1 Basi Yakobo akafahamu kwamba kuna nafaka huko Misri. Akawaambia wanawe, "Kwa nini mnatazamana?" 2 Akasema, "Tazama, nimesikia kwamba kuna nafaka huko Misri. Shukeni huko mkatununulie chakula ili tuishi wala tusife." 3 Ndugu kumi wa Yusufu wakashuka Misri kununua chakula. 4 Lakini Benjamini, ndugu wa Yusufu, Yakobo hakumtuma na ndugu zake, kwani alihofu kwamba madhara yaweza kumpata. 5 Wana wa Israeli wakaja kununua miongoni mwao waliokuja, kwani njaa ilikuwapo katika nchi ya Kanaani. 6 Basi Yusufu alikuwa mtawala juu ya nchi. Ndiye aliyekuwa akiwauzia watu wote wa nchi. Ndugu zake Yusufu wakaja na kumwinamia na nyuso zao hata chini. 7 Yusufu akawaona ndugu zake na kuwatambua, lakini alijibadili kwao na kuongea nao kwa ukali. Akawaambia, "Mmetoka wapi?" Wakasema, "Kutoka nchi ya Kanaani ili kununua chakula." 8 Yusufu akawatambua ndugu zake, lakini wao hawakumtambua. 9 Yusufu akazikumbuka ndoto alizoziota kuhusu wao. Akawaambia, "Ninyi ni wapelelezi. Mmekuja kuona sehemu za nchi zisizolindwa." 10 Wakamwambia, "Hapana, bwana wangu. Watumishi wako wamekuja kununua chakula. 11 Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Ni watu wa kweli. Watumishi wako siyo wapelelezi." 12 Akawaambia, "Hapana, mmekuja kuangalia sehemu za nchi zisizolindwa." 13 Wakasema, "Sisi watumishi wako tupo ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja katika nchi ya Kanaani. Tazama, mdogo yupo na baba yetu, na mwingine hayupo hai tena." 14 Yusufu akawaambia, "Ndivyo nilivyowaambia; ninyi ni wapelelezi. 15 Mtajaribiwa kwa njia hii. Kama aishivyo Farao, hamtaondoka hapa, mdogo wenu asipokuja hapa. 16 Mtumeni mmoja wenu amlete mdogo wenu. Mtabaki gerezani, hata maneno yenu yatakapothibitishwa, kwamba kuna ukweli ndani yenu." 17 Akawaweka kifungoni kwa siku tatu. 18 Katika siku ya tatu Yusufu akaongea nao, "Fanyeni hivi nanyi mtaishi, kwani ninamcha Mungu. 19 Kama ninyi ni watu wa kweli, mmoja wenu atazuiliwa hapa gerezani, lakini ninyi nendeni, chukueni nafaka kwa ajili ya nyumba zenu. 20 Mleteni mdogo wenu kwangu ili kwamba maneno yenu yathibitishwe nanyi hamtakufa." Wakafanya hivyo. 21 Wakasemezana wao kwa wao, "Kwa kweli tuna hatia juu ya ndugu yetu kwani tuliona taabu ya nafsi yake alipotusihi nasi hatukusikia. Kwa hiyo taabu hii imeturudia." 22 Rubeni akawajibu, "Je sikuwaambia, 'Msitende dhambi juu ya kijana,' lakini hamkusikia? Basi, tazama, damu yake inatakiwa juu yetu." 23 Lakini hawakujua kwamba Yusufu anawaelewa, kwani kulikuwa na mkalimani kati yao. 24 Akatoka kwao na kulia. Akarudi kwao na kuongea nao. Akamchukua Simoni miongoni mwao na kumfunga mbele ya macho yao. 25 Kisha Yusufu akaagiza watumishi kujaza mifuko yao kwa nafaka, na kurudisha pesa ya kila mmoja katika gunia lake, nakuwapa mahitaji kwa safari. Wakatendewa hivyo. 26 Hawa ndugu wakapandisha chakula chao juu ya punda zao na kuondoka pale. 27 Mmoja wao alipofungua gunia lake ili kumlisha punda wao katika sehemu waliyokuwa, akaona pesa yake. Tazama, ilikuwa mdomoni mwa gunia lake. 28 Akawaambia ndugu zake, "Pesa yangu imerudishwa. Tazama, imo katika gunia langu." Mioyo yao ikazimia na wakageukiana kila mmoja huku wakitetemeka. Wakasema, "Ni nini hiki alichotutendea Mungu?" 29 Wakaenda kwa Yakobo, baba yao katika nchi ya Kanaani na kumwambia yote yaliyowapata. 30 Wakasema, "Yule mtu, bwana wa nchi, aliongea nasi kwa ukali na kutudhania kuwa wapelelezi katika nchi. 31 Tukamwambia, 'Tu watu wa kweli sisi. Sisi siyo wapelelezi. 32 Tupo ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu. Mmoja hayupo hai tena, na mdogo yupo na baba yetu katika nchi ya Kanaani." 33 Yule mtu, bwana wa nchi, akatwambia, 'Kwa hili nitajua kwamba ni watu wa kweli ninyi. Mwacheni mmojawapo wa ndugu zenu, chukueni chakula kwa ajili ya njaa katika nyumba zenu, na mwondoke. 34 Mleteni mdogo wenu kwangu. Ndipo nitakapojua kwamba ninyi si wapelelezi, lakini ni watu wa kweli. Kisha nitamwachilia ndugu yenu, na mtafanya biashara katika nchi." 35 Ikawa walipoyafungua magunia yao, na tazama, kila mfuko wa fedha wa mmojawao ulikuwa katika gunia lake. Wakati wao na baba yao walipoona mifuko yao ya fedha, wakaogopa. 36 Yakobo baba yao akawambia, "Mmeniharibia watoto wangu. Yusufu hayupo hai tena, Simoni ameondoka, nanyi mmpeleke Benjamini naye. Mambo haya yote ni kunyume changu." 37 Rubeni akamwambia baba yake, kusema, "Unaweza kuwaua wanangu wawili nisipomrudisha Benjamini kwako. Mweke mikononi mwangu, nami nitamrudisha tena kwako." 38 Yakobo akasema, "Mwanangu atashuka pamoja nanyi. Kwani ndugu yake amekufa na yeye peke yake amebaki. Ikiwa madhara yatampata katika njia mnayoiendea, ndipo mtakapozishusha mvi zangu kaburini kwa huzuni."