1
Mungu akamwambia Yakobo, "Inuka, panda kwenda Betheli, na ukae pale. Unijengee madhabahu pale, niliyekutokea pale ulipomkimbia Esau kaka yako."
2
Kisha Yakobo akawaambia nyumba yake na wote aliokuwa nao, "Wekeni mbali miungu yote ya kigeni iliyo kati yenu, jitakaseni wenyewe, na kubadili mavazi yenu.
3
Kisha tuondoke na kwenda Betheli. Nitajenga pale madhabahu kwa Mungu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, naye amekuwa pamoja nami kila nilikokwenda."
4
Hivyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni iliyokuwa mikononi mwao, na heleni zilizokuwa katika masikio yao. Yakobo akazifukia chini ya mwaloni uliokuwa karibu na Shekemu.
5
Kwa kadiri walivyo safiri, Mungu akaifanya miji yote iliyokuwa karibu nao kuhofu, hivyo watu hao hawakuwafuatia wana wa Yakobo.
6
Hivyo Yakobo akafika Luzu (ndiyo Betheli), ulioko katika nchi ya Kanaani, yeye na watu wote aliokuwa nao.
7
Alijenga madhabahu na kuliita eneo hilo El Betheli, kwa sababu Mungu alikuwa amejifunua kwake, alipokuwa akimkimbia ndugu yake.
8
Debora, mlezi wa Rebeka, akafa. Akazikwa chini kutoka Betheli chini ya mwaloni, hivyo ikaitwa Aloni Bakuthi.
9
Yakobo alipokuja kutoka Padani Aramu, Mungu akamtokea tena na kumbariki.
10
Mungu akamwambia, "Jina lako ni Yakobo, lakini jina lako halitakuwa Yakobo tena. Jina lako litakuwa Israeli." Hivyo Mungu akamwita jina lake Israeli.
11
Mungu akamwambia, "Mimi ni Mungu Mwenyezi, Uwe mwenye kuzaa na kuongezeka. Taifa na wingi wa mataifa watakujia, na wafalme watatoka miongoni mwa uzao wako.
12
Nchi ambayo nilimpa Ibrahimu na Isaka, nitakupa wewe. Nami nitaupa pia uzao wako baada yako nchi hii."
13
Mungu akapanda kutoka mahali alipoongea naye.
14
Yakobo akaweka nguzo katika eneo ambalo Mungu alikuwa ameongea naye, nguzo ya jiwe. Akamimina juu yake sadaka ya kinywaji na akamimina mafuta juu yake.
15
Yakobo akaiita sehemu Mungu aliyoongea naye, Betheli.
16
Wakaendelea na safari kutoka Betheli. Walipokuwa kitambo kabla ya kufika Efrathi, Raheli akashikwa na uchungu.
17
Akawa na uchungu mzito. Alipokuwa katika uchungu mzito zaidi, mkunga akamwambia, "Usiogope, kwani sasa utapata mtoto mwingine wa kiume."
18
Hata alipokaribia kufa, kwa pumzi yake ya mwisho akamwita jina lake Benoni, lakini baba yake akamwita jina lake Benjamini.
19
Raheli akafa na kuzikwa katika njia iendayo Efrathi (ndio Bethlehemu).
20
Yakobo akaweka nguzo katika kaburi lake. Ndiyo alama ya kaburi la Raheli hata leo.
21
Israeli akaendelea na safari na akaweka hema yake kuvuka mnara wa walinzi wa kondoo.
22
Yakobo alipokuwa akiishi katika nchi hiyo, Rubeni akalala na Bilha suria wa baba yake, na Israeli akasikia kuhusu hilo. Basi Yakobo alikuwa na wana kumi na wawili.
23
Wanawe kwa Lea walikuwa Rubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, na Simoni, Lawi, Yuda, Isakari, na Zabuloni.
24
Wanawe kwa Raheli walikuwa Yusufu na Benjamini.
25
Wanawe kwa Bilha, mjakazi wa Raheli walikuwa Dani na Naftali.
26
Wana wa Zilpa, mjakazi wa Lea, walikuwa Gadi na Asheri. Hawa wote walikuwa wana wa Yakobo waliozaliwa kwake huko Padani Aramu.
27
Yakobo akaja kwa Isaka, baba yake, huko Mamre katika Kiriathi Arba (jina sawa na Hebroni), alipoishi Ibrahimu na Isaka.
28
Isaka akaishi miaka 180.
29
Isaka akapumua pumzi yake ya mwisho na akafa, na akakusanywa kwa wahenga wake, na mtu mzee amejaa siku. Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika.