1
Mfalme Nebukadneza aliituma amri hii kwa watu wote, mataifa, na lugha walioishi katika nchi: "Na amani yenu na iongezeke.
2
Imeonekana vizuri kwangu kuwaambia juu ya ishara na maajabu ambayo Mungu Mkuu Aliye juu amenifanyia.
3
Ni kwa namna gani Ishara zake ni kubwa, na ni kwa namna gani maajabu yake yana nguvu! Ufalme wake ni ufalme unaodumu milele, na utawala wake hudumu kizazi hadi kizazi."
4
Mimi, Nebukadneza, nilikuwa ninaishi kwa furaha katika nyumba yangu, na nilikuwa nikifurahia mafanikio katika ikulu yangu.
5
Lakini ndoto niliyoiota ilifanya niogope. Nilipokuwa nimejilaza pale, taswira niliyoiona na maono katika akili yangu yalinitaabisha.
6
Basi nilitoa agizo la kuwaleta mbele yangu watu wote wa Babeli waliokuwa na hekima ili kwamba waweze kunitafsiria ndoto.
7
Kisha walikuja wachawi, wale ambao hudai kuzungumza na wafu, watu wenye hekima, na wasoma nyota. Niliwaambia juu ya ndoto, lakini hawakuweza kunitafsiria.
8
Bali mwishoni Danieli aliingia ndani - yeye ambaye huitwa Belteshaza jina la mungu wangu, na ambaye ndani yake kuna roho ya miungu mitakatifu - na nilimwambia juu ya ndoto.
9
"Belteshaza, mkuu wa wachawi, ninajua kuwa roho ya miungu watakatifu iko ndani yako na ya kwamba hakuna siri iliyo ngumu kwako. Niambie kile nilichokiona katika ndoto yangu na nini maana yake.
10
Haya ndiyo niliyoyaona katika akili zangu nilipokuwa nimejilaza katika kitanda changu: Nilitazama, na kulikuwa na mti katikati ya dunia, na urefu wake ulikuwa ni mkubwa sana.
11
Mti ulikua na ukawa wenye nguvu. Na sehemu ya juu yake ilifika mbinguni, uliweza kuonekana kutoka miisho ya dunia yote.
12
Majani yake yalikuwa mazuri, matunda yake yalikuwa ni mengi, na juu yake kulikuwa na chakula kwa ajili ya wote. Wanyama wa mwituni walipata kivuli chini yake, na ndege wa angani waliishi katika matawi yake. Viumbe vyote hai viliishi katika mti huo.
13
Nilipokuwa nimelala kitandani kwangu, niliona katika akili zangu, mjumbe mtakatifu alishuka kutoka mbinguni.
14
Alipiga kelele na kusema, 'Ukateni mti na yafyekeni matawi yake, yapukutisheni majani yake, na kuyasambaza matunda yake.
15
Mkiache kisiki cha mizizi yake katika nchi, mkifunge na pingu ya chuma na shaba, katikati ya mche mororo wa shambani. Na kilowanishwe na umande wa kutoka mbinguni. Kiacheni kiishi na wanyama kati ya mimea ya ardhini.
16
Akili yake na ibadilishwe kutoka akili ya kibinadamu, na apewe akili ya mnyama mpaka ipite miaka saba.
17
Uamuzi huu ni kutokana na amri iliyotolewa na mjumbe. Ni uamuzi uliofanya na yeye aliye mtakatifu ili kwamba hao walio hai wajue kwamba Mungu aliye juu sana anatawala juu ya falme za watu na huwapa kwa kila mmoja apendaye kumweka juu yao, hata kwa watu wale wanyenyekevu sana.'
18
Mimi, Mfalme Nebukadneza nilipata ndoto hii. Sasa, wewe Belteshaza, niambie tafsiri yake, kwa sababu hakuna mtu mwenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunitafsiria. Lakini wewe unaweza kufanya hivyo, kwa kuwa roho ya miungu watakatifu iko ndani yako."
19
Ndipo Danieli aliyeitwa pia Belteshaza, alihuzunishwa kwa muda, na mawazo yake yalimshitua. Mfalme akasema, " Belteshaza, usifadhaishwe na ndoto au tafsiri yake." Belteshaza akajibu, " Bwana wangu, ndoto hii na iwe kwa ajili ya watu wanaokuchukia, na tafsiri yake na iwe kwa ajili ya adui zako.
20
Mti ule uliouona - uliokua na ukawa na wenye nguvu, na ambao sehemu yake ya juu ilifika hata mbinguni, na ambao waweza kuonekana kutoka miisho ya dunia yote -
21
ambao majani yake ni mazuri, na matunda yake yalikuwa ni mengi, ili kwamba ndani yake kulikuwa na chakula cha wote, na chini yake wanyama wa mwituni walipata kivuli, na ndani yake ndege wa angani waliishi -
22
huu mti ni wewe, mfalme, wewe uliyekua na kuwa na nguvu. Ukuu wako umeongezeka na kufika mbinguni, na mamlaka yako yamefika hata miisho ya dunia.
23
Ewe mfalme, ulimwona mjumbe akishuka kutoka mbinguni na akisema, "Ukateni mti na uteketezeni, lakini kiacheni kisiki cha mizizi yake katika nchi, kifungeni kwa ukanda wa chuma na shaba, katikati ya mche mororo katika shamba. Na kilowanishwe na umande kutoka mbinguni. Kiache kiishi katika wanyama wa mwituni katika mashamba mpaka ipite miaka saba.'
24
Mfalme, hii ni tafsiri yake. Ni agizo la Yeye Aliye Juu ambalo limekufikia, bwana wangu mfalme.
25
Utafukuzwa utoke miongoni mwa watu, na utaishi pamoja na wanyama wa mwituni huko mashambani. Utafanywa uwe unakula majani kama ng'ombe, na utalowanishwa na umande wa kutoka mbinguni, miaka saba itapita mpaka pale utakapokiri kwamba Mungu Aliye Juu anatawala juu ya falme zote za watu na ya kwamba yeye humpa falme hizo mtu yeyote amtakaye.
26
Kama ilivyoamriwa kwamba kukiacha kisiki cha mizizi ya mti, kwa njia hii ufalme wako utarudishiwa katika kipindi ambacho utajifunza kwamba mbingu inatawala.
27
Hivyo basi, mfalme, ushauri wangu na ukubalike kwako. Acha kutenda dhambi na utende haki. Geuka uache uovu wako wa kuonesha huruma kwa walionewa, na itakuwa kwamba mafanikio yako yataongezwa."
28
Vitu hivi vyote vilitokea kwa mfalme Nebukadneza.
29
Baada ya miezi kumi na miwili alipokuwa akitembea juu ya dari la ikulu ya kifalme katika Babeli,
30
na alisema, " Je, hii si Babeli kuu, ambayo nimeijenga kwa ajili ya makao yangu ya kifalme, kwa ajili ya utukufu wa enzi yangu?"
31
Wakati maneno yakali katika midomo ya mfalme, sauti ilisikika kutoka mbinguni: "Mfalme Nebukadneza, imetangazwa kwako kwamba ufalme huu umeondolewa kutoka kwako.
32
Utafukuziwa mbali kutoka miongoni mwa watu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa mwitu katika mashamba. Utafanywa kula majani kama ng'ombe. Miaka saba itapita mpaka pale utakapokiri kwamba Mungu Aliye Juu anatawala juu ya falme za watu na humpa falme mtu yeyote amtakaye.
33
Agizo hili kinyume na Nebukadneza lilitekelezwa ghafla. Aliondolewa miongoni mwa watu. Alikula majani kama ng'ombe, na mwili wake ulilowa kwa umande wa kutoka mbinguni. Nywele zake zilirefuka kama manyoa ya tai, na makucha yake yalikuwa kama makucha ya ndege.
34
Na katika mwisho wa siku, mimi, Nebukadneza niliinua macho yangu kuelekea mbinguni, utimamu wa akili nilirudishiwa. "Nilimsifu Mungu Aliye Juu sana, na nilimheshimu na kumtukuza yeye aishiye milele. Kwa kuwa utawala wake ni wa milele, na ufalme wake unadumu katoka katika vizazi vyote hadi vizazi vyote.
35
Wenyeji wote wa duniani huhesabiwa na yeye kuwa bure; hufanya lolote limpendezalo miongoni mwa jeshi la mbinguni na wakazi wa dunia. Hakuna hata mmoja awezaye kumzuia au kumpa changamoto. Hakuna hata mmoja awezaye kumwambia, "Mbona umefanya hivi?"
36
Kwa wakati ule ule utimamu wa akili zangu uliponirudia, utukufu wangu na fahari yangu ilinirudia kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu. Washauri wangu na watu wenye heshima walitafuta msaada wangu. Nilirudishwa kwenye kiti changu cha enzi, na nilipewa ukuu zaidi.
37
Sasa basi, mimi Nebukadneza, ninamsifu, ninamtukuza na kumheshimu mfalme wa mbinguni, kwa kuwa matendo yake yote ni ya haki, na njia zake ni za adili. Anaweza kuwashusha wale wanaotembea katika kiburi chao wenyewe.