Sura 12

1 Wakati huo mfalme Herode alinyosha mkono wake kwa baadhi ya watu wa kanisa ili apate kuwatesa. 2 Akamwuua Yakobo nduguye Yohana kwa upanga. 3 Baada ya kuona kwamba hili liliwapendeza Wayahudi, alimkamata Petro.Hii ilikuwa wakati wa siku za mikate isiyotiwa chachu. 4 Alipomkamata, akamweka gerezani na akamweka  chini ya vikosi vinne vya askari ili kumlinda, alikuwa akitarajia kumpeleka kwa hadhara baada ya Pasaka. 5 Petro akawekwa gerezani, lakini maombi yalifanywa kwa bidii na kanisa kwa ajili yake kwa Mungu. 6 Usiku huo kabla Herode hajaenda kumtoa, kwa ajili ya kesi, Petro alikuwa amelala katikati ya maaskari wawili, akiwa amefungwa na minyororo miwili, huku walinzi wakiwa mbele ya mlango wakilinda gereza. 7 Tazama, Malaika wa Bwana ghafla akamtokea na nuru ikang'aa ndani ya gereza. Akampiga Petro ubavuni na kumwamsha akisema, "Amka haraka." na  minyororo aliyokuwa amefungwa ikaanguka kutoka mikononi mwake. 8 Malaika akamwambia, "Vaa nguo zako na vaa viatu vyako." Petro akafanya hivyo. Malaika akamwambia, "Vaa koti lako na unifuate." 9 Hivyo Petro akamfuata Malaika na akatoka nje. Hakujua kama kilichofanywa na malaika ni cha kweli. Alidhani anaona maono. 10 Baada ya kupita lindo la kwanza na la pili, wakafika kwenye lango la chuma la kuingilia kwenda mjini, likafunguka lenyewe kwa ajili yao. Wakatoka nje na wakashuka kwenye mtaa, mara Malaika akamwacha. 11 Petro alipojitambua, akasema, "Sasa nimeamini kwa kweli Bwana alimtuma Malaika wake ili kunitoa katika mkono wa Herode, na kwa matarajio ya watu wote wa uyahudi." 12 Baada ya kujua haya, akaja kwenye nyumba ya Mariamu mama yake Yohana ambaye pia huitwa Marko; ambako Wakristo wengi walikuwa wamekusanyika wakiomba. 13 Alipobisha kwenye mlango wa lango, mtumishi mmoja msichana anayeitwa Roda akaja kufungua. 14 Alipotambua ni sauti ya Petro, kwa furaha akashindwa kuufungua mlango; badala yake, akakimbia ndani ya chumba; na kuwajulisha kuwa Petro amesimama mbele ya Mlango. 15 Hivyo, Wakasema kwake, "Wewe ni mwendawazimu" lakini alikazia kuwa kwa kweli ni yeye. Wakasema "Huyo ni malaika wake." 16 Lakini Petro aliendelea kubisha, na walipofungua mlango, wakamwona na wakashangaa sana. 17 Petro akawaashiria kwa mkono wakae kimya na akawaambia jinsi Bwana alivyomtoa kutoka Gerezani. akasema,"Wajulishe haya mambo Yakobo na ndugu zake." Kisha akaondoka akaenda sehemu nyingine. 18 Sasa kulipokuwa mchana, kukawa na vurugu si kidogo kati ya askari, uhusiana na kilichotokea kwa Petro. 19 Baada ya Herode kumtafuta na kutompata akawauliza walinzi na akaamuru wauwawe. Akaenda kutoka uyahudi mpaka Kaisaria na kukaa huko. 20 Ikawa Herode alikuwa na hasira juu ya watu wa Tiro na Sidoni. Wakaenda kwake kwa nia moja na baada ya kumshawishi Blasto,aliyekuwa msaidizi wa mfalme Herode kuwa urafiki nao, waliomba awasaidie. Waliomba amani kwa sababu nchi yao ilipokea chakula kutoka nchi ya mfalme. 21 Siku iliyokusudiwa Herode alivaa mavazi ya kifalme na kukaa kwenye kiti chake cha kifalme, na akawahutubia. 22 Watu wakapasa sauti,"Hii ni sauti ya mungu wala si sauti ya mwanadamu!" 23 Mara hiyo hiyo malaika akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango na akafa 24 Lakini neno la Mungu likakua na kusambaa. 25 Basi ikawa Barnaba na Sauli walipokamilisha huduma yao pale wakarejea Yerusalemu huku wakimchukua pamoja nao Yohana aaitwaye Marko.