Sura 19

1 Yoabu akaambiwa, "Tazama, mfalme analia na kumuomboleza Absalomu." 2 Hivyo siku ile ushindi uligeuzwa kuwa maombolezo kwa jeshi lote, kwa maana jeshi likasikia ikisemwa siku hiyo, "Mfalme anaomboleza kwa ajili ya mwanaye." 3 Siku ile askari waliingia mjini kwa kunyemelea kimyakimya kama watu waonao haya baada ya kukimbia vitani. 4 Mfalme akafunika uso wake na kulia kwa sauti, "Mwanangu Absalomu, Absalomu, mwanangu, mwangangu!" 5 Ndipo Yoabu akaingia ndani kwa mfalme na kumwambia, "Leo umeziaibisha nyuso za askari wako, waliookoa maisha yako leo, maisha ya wanao na binti zako, maisha ya wake zako na maisha ya masuria wako, 6 kwa maana wawapenda wakuchukiao na kuwachukia wakupendao. Kwa kuwa leo umeonyesha kwamba maakida na askari si chochote kwako. Natambua sasa kwamba kama Absalomu angesalia na sisi sote tungekufa hilo lingekufurahisha. 7 Sasa basi, inuka na uende kuongea na askari wako kwa upole, kwani nakuapia kwa Yahwe, ikiwa hutakwenda hakuna mtu hata mmoja atakayesalia nawe usiku huu. Na hii itakuwa vibaya sana kwako kuliko madhara yoyote yaliyowai kukupata tangu ujana wako." 8 Hivyo mfalme akainuka na kuketi kati ya lango la mji, watu wote wakaambiwa, "Tazama, mfalme ameketi kati ya lango." Ndipo watu wote wakaja mbele za mfalme. Walakini, Israeli walikuwa wamekimbia kila mtu hemani mwake. 9 Watu wote wakahojiana wao kwa wao katika jamaa zote za Israeli wakisema, "Mfalme alituokoa na mkono wa adui zetu. Alitukomboa na mkono wa Wafilisti lakini sasa ameikimbia nchi mbele ya Absalomu. 10 Na Absalomu tuliyemtia mafuta juu yetu amekufa vitani. Hivyo kwa nini hatuongei juu ya kumrudisha mfalme tena?" 11 Mfalme Daudi akatuma kwa Sadoki na kwa Abiathari makuhani akisema, "Ongeeni na wazee wa Yuda mkisema, Kwa nini ninyi mmekuwa wa mwisho kumrudisha mfalme kwenye kasri lake tena, kwa vile usemi wa Israeli wote unamtaka mfalme arudi katika kasri lake? 12 Ninyi ni ndugu zangu, mwili na mifupa yangu. Kwa nini basi mmekuwa wa mwisho kumrudisha mfalme?" 13 Na mwambieni Amasa, "Je wewe si mwili na mfupa wangu? Mungu anifanyie hivyo na kuzidi pia ikiwa hautakuwa jemedari wa jeshi langu tangu sasa na baadaye mahali pa Yoabu. 14 Naye akaishinda mioyo ya watu wote wa Yuda kama mtu mmoja. Wakatuma kwa mfalme wakisema, "Rudi sasa na watu wako wote." 15 Hivyo mfalme akarudi naye akaja Yordani. Na watu wa Yuda wakaja Gilgali kwenda kumlaki mfalme ili kumvusha mfalme juu ya Yordani. 16 Shimei mwana wa Gera, Mbenjamini, kutoka Bahurimu, akaharakisha kushuka pamoja na watu wa Yuda ili kumlaki mfalme Daudi. 17 Kulikuwa na watu 1,000 kutoka Benjamini waliokuwa pamoja naye, na Siba mtumishi wa Sauli na wanawe kumi na watano na watumishi wake ishirini walikuwa pamoja naye. Wakavuka Yordani mbele za mfalme. 18 Wakavuka ili kuivusha familia ya mfalme na kumfanyia lolote aliloona jema. Shimei mwana wa Gera akainama chini mbele za mfalme mara alipoanza kuuvuka Yordani. 19 Shimei akamwambia mfalme, "Bwana wangu asinione mwenye hatia au kuyaweka moyoni ambayo mtumishi wake alifanya kwa ukaidi siku bwana wangu mfalme alipoondoka Yerusalemu. Tafadhali, mfalme na asiyaweke moyoni. 20 Kwa maana mtumishi wako anatambua kwamba amekosa. Tazama, ndiyo maana nimekuja leo wa kwanza katika nyumba ya Yusufu ili kumlaki bwana wangu mfalme." 21 Lakini Abishai mwana wa Seruya akajibu na kusema, "Je Shimei asife kwa hili kwa vile alivyomlaani mtiwa mafuta wa Yahweh?" 22 Ndipo Daudi akasema, "Nifanye nini nanyi enyi wana wa Seruya, hata leo mkawa adui zangu? Je mtu yeyote atauawa leo katika Israeli? Kwani sijui kama leo mimi ni mfalme juu ya Israeli? 23 Hivyo mfalme akamwambia Shimei, "Hautakufa." Mfalme akamuahidi kwa kiapo. 24 Kisha Mefiboshethi mwana wa Sauli akashuka ili kumlaki mfalme. Hakuwa ameivalisha miguu yake wala kunyoa ndevu zake wala kufua nguo zake tangu siku mfalme alipoondoka hata siku aliporudi kwa amani. 25 Na hivyo alipotoka Yerusalemu ili kumlaki mfalme, mfalme akamwambia, "Mefiboshethi kwa nini haukwenda pamoja nami?" 26 Akajibu, "Bwana wangu mfalme mtumishi wangu alinidanganya, kwani nilisema, nitapanda juu ya punda ili niende na mfalme, kwa kuwa mtumishi wako ni mlemavu.' 27 Mtumishi wangu Siba amenisemea uongo, mtumishi wako, kwa bwana wangu mfalme. Lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu. Kwa hiyo fanya lililojema machoni pako. 28 Kwa maana nyumba yote ya baba yangu walikuwa maiti mbele ya bwana wangu mfalme, lakini ukamuweka mtumishi wako miongoni mwao walao mezani pako. Kwa hiyo nililiye haki gani zaidi kwa mfalme?" 29 "Kisha mfalme akamwambia, "Kwa nini kueleza yote zaidi? Nimekwisha amua kwamba wewe na Siba mtagawana mashamba." 30 Ndipo Mefiboshethi akamjibu mfalme, "Sawa, acha achukue yote kwa vile bwana wangu mfalme amerudi salama nyumbani kwake." 31 Kisha Berzilai Mgileadi akashuka kutoka Rogelimu ili avuke Yordani pamoja na mfalme, naye akamsaidia mfalme kuuvuka Yordani. 32 Basi Berzilai alikuwa mzee sana mwenye umri wa miaka themanini. Alikuwa amemsaidia mfalme kwa mahitaji alipokuwako Mahanaimu kwani alikuwa na mali nyingi. 33 Mfalme akamwambia Berzilai, njoo pamoja nami, nami nitakupa riziki ukae nami huko Yerusalemu." 34 Berzilai akamjibu mfalme, "Kwani kuna siku ngapi zilizosalia maishani mwangu, hata niende na mfalme huko Yerusalemu? 35 Nina umri wa miaka themanini. Je, naweza kutofautisha mema na mabaya? Je, mtumishi wako anaweza kuonja anachokula au kunywa? Je, naweza kusikia sauti zaidi za wanaume na wanawake waimbao? Kwa nini basi mtumishi wako awe mzigo kwa bwana wangu mfalme? 36 Mtumishi wako angependa tu kuvuka Yordani pamoja na mfalme. Kwa nini mfalme anilipe kwa thawabu kama hiyo? 37 Tafadhali mruhusu mtumishi wako arudi nyumbani, ili kwamba nife katika mji wangu katika kaburi la baba na mama yangu. Lakini tazama, huyu hapa mtumishi wako Kimhamu. Haya yeye na avuke na bwana wangu mfalme na umfanyie lolote lipendezalo kwako." 38 Mfalme akajibu, "Kimhamu atakwenda pamoja nami, nami nitamtendea kila lionekanalo jema kwako, na lolote unalotamani kutoka kwangu nitakutendea." 39 Kisha watu wote wakavuka Yordani, mfalme naye akavuka, kisha mfalme akambusu Berzilai na kumbariki. Kisha Berzilai akarudi nyumbani kwake. 40 Hivyo mfalme akavuka kuelekea Gilgali, na Kimhamu akavuka pamoja naye. Jeshi la Yuda lote na nusu ya jeshi la Israeli likamleta mfalme. 41 Mara watu wa Israeli wote wakaanza kuja kwa mfalme na kumwambia, "Kwa nini ndugu zetu, watu wa Yuda, wamemuiba na kumleta mfalme na familia yake juu ya Yordani na watu wote wa Daudi pamoja naye?" 42 Hivyo watu wa Yuda wakawajibu watu wa Israeli, "Ni kwa kuwa mfalme anahusiana nasi kwa karibu zaidi. Kwa nini basi mkasirike juu ya hili? Je sisi tumekula chochote ambacho mfalme amekitoa? Je ametupa zawadi yoyote?" 43 Watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, "Sisi tuna kabila kumi zaidi kwa mfalme hivyo tuna sehemu kubwa zaidi kwa Daudi kuliko ninyi. Kwa nini basi mlitudharau? Je hatukuwa wa kwanza kupendekeza kumrudisha mfalme wetu?" Lakini maneno ya watu wa Yuda hata yakawa makali kuliko maneno ya watu wa Israeli.