1
Beni Hadadi mfalme wa Shamu akakusanya jeshi lake lote pamoja. Kulikuwa na wafalme thelathini na mbili wasaidizi pamoja naye, na magari na farasi. Akapanda, akaihusuru Samaria na kupigana nayo.
2
Akatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, akamwambia, "Beni Hadadi anasema hivi:
3
Fedha zako na dhahabu zako ni zangu. Pia wake zako na watoto, wale wazuri, sasa ni wangu."
4
Mfalme wa Israeli akajibu akasema, "Na iwe kama unavyosema, bwana wangu, mfalme. Mimi pamoja na vile nilivyo navyo ni mali yako."
5
Wale wajumbe wakaja tena wakasema, "Beni Hadadi anasema hivi, 'Nilituma neno kwako nikisema kwamba lazima ukabidhi kwangu fedha zako, dhahabu zako, wake zako na watoto wako.
6
Lakini kesho nitatuma watumishi wangu kwako wakati kama huu, nao wataichunguza nyumba yako na nyumba za watumishi wako. Nao watatia mikononi mwao na kukichukua kila wakipendacho machoni mwao.'"
7
Ndipo mfalme wa Israeli akawaita wazee wote wa nchi pamoja akawaambia, ''Hebu angalieni jinsi huyu mtu anavyotafuta matatizo. Amenitumia ujumbe kwamba anataka kuchukua wake zangu, watoto wangu, fedha na dhahabu zangu, nami sijamkatalia."
8
Wazee wote na watu wote wakamwambia Ahabu, "Usimsikilize wala kukubaliana na matakwa yake."
9
Ahabu akawaambia wajumbe wa Beni Hadadi, "Mwambieni bwana wangu mfalme kwamba, 'Ninakubaliana na kila kitu ambacho kwanza uliwatuma watumishi wako kufanya kwangu, lakini sikubaliani na matakwa yako haya ya pili.'" Wale watumishi wa Beni Hadadi wakaondoka wakampelekea mrejesho Beni Hadadi.
10
Naye Beni Hadadi akatuma tena majibu yake kwa Ahabu, akasema, "Basi miungu inifanyie hivyo na zaidi, kama hata mavumbi ya Samaria yatawatosheleza watu wote wanaonifuata kuchukua kila mmoja angalau konzi mkononi mwake."
11
Naye mfalme wa Israeli akamjibu akisema, "Mwambieni Beni Hadadi, 'Hakuna abebaye silaha yake, atakayejivuna kama wakati wa kuishusha."'
12
Beni Hadadi aliusikia ujumbe huu wakati alipokuwa akinywa, yeye na wafalme walikuwa pamoja naye waliokuwa kwenye mahema yao. Beni Hadadi akayaamuru majeshi yake, "Jipangeni katika sehemu zenu kwa ajili ya vita." Kwa hiyo wakajiandaa kivita ili kuuvamia mji.
13
Tazama, nabii akaja kwa Ahabu mfalme wa Israeli akasema, "BWANA asema, 'Je umeliona hili jeshi kubwa? Tazama, nitaliweka katika mkono wako leo, nawe utatambua kuwa mimi ni BWANA.'"
14
Naye Ahabu akajibu, ''kwa nani? BWANA akamjibu akasema, "kwa kuwatumia vijana wanaotumikia maliwali wa wilaya." kisha Ahabu akasema, "Ni nani atakayepewa hiyo vita?' BWANA akamwambia, "Wewe."
15
Ndipo Ahabu alipowataarifu wale vijana wanaowatumikia maliwali wa wilaya. Idadi yao ilikuwa mia mbili therathini na mbili. Baada yao aliwahesabu wanajeshi wote, jeshi lote la Israeli; idadi yao ilikuwa elfu saba.
16
Nao wakatoka wakati wa adhuhuri. Naye Beni Hadadi alikuwa akinywa na kulewa hemani mwake, yeye na wale wafalme wadogo thelathini na mbili waliokuwa wakimsaidia.
17
Wale maakida vijana waliokuwa wakiwasaidia maliwali wa wilaya walitangulia kwanza. Kisha Beni Hadadi alitaarifiwa na wanaskauti aliokuwa amewatuma kwamba, "kuna watu wanakuja kutoka Samaria."
18
Beni Hadadi akasema, "Wawe wamekuja kwa amani au kwa vita, wakamateni wakiwa hai."
19
Kwa hiyo wale vijana wanaowatumikia maliwali wa wilaya wakaenda mjini na jeshi likawafuata kwa nyuma.
20
Kila mmoja akaua adui wake na wale washami wakakimbia. Israeli ikawashinda. Beni Hadadi mfalme wa Shamu akatoroka kwa farasi pamoja na wapanda farasi.
21
Kisha mfalme wa Israeli akaenda akawashambulia farasi na magari, na kuwaua washami kwa mauaji makubwa.
22
Yule nabii akaja kwa mfalme wa Israeli akamwambia, "Nenda, ukajiimarishe mwenyewe, uelewa na kupanga kile unachofanya, kwa sababu mwakani mfalme wa Shamu atapanda dhidi yako tena."
23
Wale watumishi wa mfalme wa Shamu wakamwambia, "Mungu wao ni mungu wa milimani. Hiyo ndiyo sababu walikuwa na nguvu kuliko tulivyokuwa. Lakini sasa hebu tupigane nao katika nchi tambarare, na kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko wao.
24
Na ufanye hivi waondoe wafalme; mwondoe kila mmoja mahali pake ukaweke majemedari mahali pao.
25
Kisha ujihesabie jeshi kama lile jeshi ulilopoteza, farasi kwa farasi na gari kwa gari, nasi tutapigana nao katika nchi tambarare, Kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko walivyo." Kwa hiyo Beni Hadadi akausikiliza ushauri huo naye akafanya kama alivyoshauriwa.
26
Baada ya mwanzo wa mwaka mpya, Beni Hadadi akawahesabu Washami na akapanda Afeki kupigana na Israeli.
27
Watu wa Israeli walikuwa
amehesabiwa na walikuwa wamejipanga kupigana nao. Watu wa Israeli wakafanya kambi mbele yao kama makundi mawili madogo ya mbuzi, lakini Washami wakaujaza upande wa nchi.
28
Ndipo mtu wa Mungu akaja karibu akaongea mfalme wa Israeli akamwambia, "BWANA anasema: 'Kwa kuwa Washami wamesema kuwa BWANA ni mungu wa milima, na wala si mungu wa mabondeni, nitaliweka hili jeshi kubwa mkononi mwako, nawe utajua kuwa mimi ni BWANA.'"
29
Kwa hiyo majeshi yakaweka kambi yakikabiliana kwa muda wa siku saba. Kisha siku ya saba vita vikaanza. Watu wa Israeli wakawaua Washami 100,000 wanajeshi wa ardhini kwa siku moja.
30
Waliobaki wakakimbilia Afeki, mjini, na ule ukuta ukaanguka juu ya watu ishirini na saba elfu waliobaki. Naye Beni Hadadi akakimbilia mjini. akaingia kwenye chumba cha ndani.
31
Wale watumishi wa Beni Hadadi wakamwambia, "Tazama sasa, tumesikia kwamba wale wafalme wa nyumba ya Israeli ni wenye rehema. Tafadhali hebu tuvaeni magunia viunoni mwetu na kamba vichwani mwetu, na twendeni kwa mfalme wa Israeli. Labda atakuokoa roho yako."
32
Kwa hiyo wakavaa magunia viunoni mwao na kujifunga kamba vichwani mwao na kisha wakaenda kwa mfalme wa Israeli wakamwambia, "Mtumishi wako Beni Hadadi, anasema, 'Tafadhali niachie uhai wangu." Ahabu akawaambia, "Je, bado yuko hai? Yeye ni ndugu yangu."
33
Sasa wale watu walikuwa wakisikiliza ishara yeyote kutoka kwa Ahabu, kwa hiyo wakamjibu haraka, "Ndiyo ndugu yako Beni Hadadi bado yuko hai." Ahabu akawaambia, "Nendeni mkamlete." Ndipo Beni Hadadi alipokuja kwake, na Ahabu akamwacha aje kwenye gari lake.
34
Beni Hadadi akamwambia Ahabu, "Nitakurudishia miji yako ambayo baba yangu alichukua toka kwa baba yako, na unaweza kutengeneza masoko kwa ajili yako Dameski, kama baba yangu alivyofanya kule Samaria." Ahabu akajibu, "Nitakuacha uende kwa agano hili." Kwa hiyo Ahabu akafanya agano naye kisha akamwacha aende.
35
Mtu mmoja, mmoja wana wa wana wa manabii, akamwambia mmoja wa wale manabii wenzake kwa neno la BWANA, "Tafadhali nipige." Lakini yule mtu akakataa kumpiga.
36
Kisha yule nabii akamwambia nabii mwenzake, " Kwa sababu umekataa kutii sauti ya
BWANA, mara tu utakaponiacha, simba atakuua." na mara tu baada ya yule mtu kumwacha, simba akamkuta na kumwua.
37
Kisha yule nabii akamkuta mtu mwingine akamwambia, "Tafadhali nipige." Yule mtu akampiga na kumwumiza.
38
Kisha yule nabii akaondoka akaenda kumsubiri yule mfalme barabarani; naye alikuwa amejibadilisha kwa kilemba machoni pake.
39
Ikawa mfalme alipokuwa akipita, Yule nabii akamwita mfalme na kumwambia, "Mtumishi wako alienda katikati ya pigano, na askari akasimama akamleta adui kwangu akasema, 'Mwangalie mtu huyu. Na ikiwa kwa vyovyote atatoroka, basi maisha yako yatatolewa kwa ajili ya maisha yake vinginevyo utalipa kilo thelathini za fedha.
40
Lakini kwa kuwa mtumishi wako alikuwa na mambo mengi akienda huku na kule, yule askari adui akatoroka." Basi mfalme wa Israeli akamwambia, "Hivyo ndivyo itakavyokuwa hukumu yako umejihukumu mwenyewe."
41
Ndipo yule nabii alipoondoa haraka kile kilemba machoni pake, na mfalme wa Israeli alipotambua kuwa huyo alikuwa mmoja wa manabii.
42
Yule nabii akamwambia mfalme, "BWANA anasema, 'Kwa sababu umemwachia aende mtu yule niliyekuwa nimemhukumu kifo, maisha yako yatachukua nafasi ya maisha yake.'"
43
Kwa hiyo mfalme wa Israeli akaenda nyumbani kwake akiwa na moyo mzito na mwenye hasira, akafika Samaria.