Sura 29
1
Kisha Yakobo akaendelea na safari yake na akafika katika nchi ya watu wa mashariki.
2
Hata alipotazama, akaona kisima kondeni, na, tazama, makundi matatu ya kondoo yalikuwa yamelala kando yake. Kwani kutoka katika hicho wangeyanywesha makundi, na jiwe juu ya mdomo wa kisima lilikuwa kubwa.
3
Wakati makundi yote yangekusanyika pale, wachungaji wangevingirisha jiwe kutoka katika mdomo wa kisima na kuwanywesha kondoo, na kisha kurudisha jiwe juu ya mdomo wa kisima, mahali pake.
4
Yakobo akawambia, “Ndugu zangu, ninyi mnatokea wapi?” Nao wakasema, “Tunatoka Harani.”
5
Akawaambia, “Mnamfahamu Labani mwana wa Nahori?” Wakasema, “Tunamfahamu.”
6
Akawaambia, “Je hajambo?” Wakasema, “Hajambo, na, tazama pale, Raheli binti yake anakuja na kondoo.”
7
Yakobo akasema, “Tazama, ni mchana. Siyo wakati wa kukusanya kondoo pamoja. Mnapaswa kuwanywesha kondoo na kisha mkaenda na kuwaacha wachunge.”
8
Wakamwambia, “Hatuwezi kuwanywesha mpaka makundi yote yakusanyike pamoja. Ndipo wanaume watakapovingirisha jiwe kutoka mlangoni mwa kisima, na ndipo tutakapowanywesha kondoo.”
9
Wakati bado Yakobo anaongea nao, Raheli akaja pamoja na kondoo wa babaye, kwani alikuwa akiwachunga.
10
Yakobo alipomwona Raheli, binti wa Labani, kaka wa mamaye, na kondoo wa Labani, kaka wa mama yake, Yakobo akaja juu, akalivingirisha jiwe kutoka mlangoni mwa kisima, na akawanywesha kondoo wa Labani, kaka wa mama yake.
11
Yakobo akambusu Raheli na akalia kwa sauti.
12
Yakobo akamwambia Raheli kwamba alikuwa ni ndugu wa baba yake, na kwamba alikuwa mwana wa Rebeka. Kisha yeye akakimbia kumwambia baba yake.
13
Labani aliposikia habari kuhusu Yakobo mwana wa dada yake, akaenda kukutana naye, akamkumbatia, akambusu, na kumleta nyumbani kwake. Yakobo akamwambia Labani mambo haya yote.
14
Labani akamwambia, “Kwa hakika wewe ni mfupa wangu na nyama yangu.” Kisha Yakobo akakaa naye kama mwezi mmoja.
15
Kisha Labani akamwambia Yakobo, “Je unitumikie bure kwa kuwa wewe ni ndugu yangu? Niambie, ujira wako utakuwaje?
16
Basi Labani alikuwa na binti wawili. Jina la mkubwa lilikuwa ni Lea, na jina la mdogo lilikuwa Raheli.
17
Macho ya Lea yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo na mwonekano.
18
Yakobo alimpenda Raheli, hivyo akasema, “Nitakutumikia miaka saba kwa ajili ya Raheli, binti yako mdogo.”
19
Labani akasema, “Itakuwa vema kukupa wewe, kuliko kumpa mtu mwingine. Kaa nami.”
20
Hivyo Yakobo akamtumikia kwa miaka saba kwa ajili ya Raheli; nayo ilionekana kwake kama siku chache tu, kwa ajili ya upendo aliokuwa nao kwake.
21
Kisha Yakobo akamwambia Labani, “Nipe mke wangu, kwani siku zangu zimetimia - ili kwamba nimwoe!
22
Hivyo Labani akawaalika watu wa mahali hapo na kuandaa sherehe.
23
Wakati wa jioni, Labani akamchukua Lea binti yake mkubwa na kumleta kwa Yakobo, aliyelala naye.
24
Labani akampa mtumishi wake wakike Zilpa kuwa mjakazi wa Lea.
25
Ilipofika asubuhi, tazama, kumbe ni Lea! Yakobo akamwambia Labani, “Ni nini hiki ulichonifanyia? Je sikukutumikia kwa ajili ya Raheli? Kwa nini basi umenihadaa?”
26
Labani akamwambia, “Siyo utamaduni wetu kumtoa binti mdogo kabla ya mzaliwa wa kwanza.
27
Timiza juma la bibi arusi, na tutakupa yule mwingine pia kwa mbadala wa kunitumikia miaka mingine saba.”
28
Yakobo akafanya hivyo, na akatimiza juma la Lea. Kisha Labani akampa Raheli binti yake kuwa mke wake.
29
Lakini pia Labani akampa Raheli binti yake Bilha, kuwa mjakazi wake.
30
Hivyo Yakobo akalala na Raheli, pia, lakini akampenda Raheli zaidi ya Lea. Hivyo Yakobo akamtumikia Labani kwa miaka saba mingine.
31
Yahwe akaona kwamba Lea hakupendwa, hivyo akalifungua tumbo lake, lakini Raheli hakuwa na mtoto.
32
Lea akashika mimba na kuzaa mwana, naye akamwita Rubeni. Kwani alisema, “Kwa sababu Yahwe ameliangalia teso langu; bila shaka mme wangu sasa atanipenda.”
33
Kisha akashika mimba tena na kuzaa mwana. Akasema, “Kwa sababu Yahwe amesikia kwamba sipendwi, kwa hiyo amenipa mwana mwingine,” na akamwita Simoni.
34
Kisha akashika mimba tena na kuzaa mwana. Akasema, “Wakati huu mme wangu ataungana nami, kwa kuwa nimemzalia wana watatu.” Kwa hiyo akaitwa Lawi.
35
Akashika mimba tena na kuzaa mwana. Akasema, “Wakati huu nitamsifu Yahwe.” Kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; kisha akaacha kuzaa watoto.