1
Malaika wawili wakaja Sodoma jioni, wakati ambao Lutu alikuwa amekaa langoni mwa Sodoma. Lutu akawaona, akainuka kuwalaki, na akainama uso wake chini ardhini.
2
Akasema, “Tafadhali Bwana zangu, nawasihi mgeuke mwende kwenye nyumba ya mtumishi wenu, mlale pale usiku na muoshe miguu yenu. Kisha muamke asubuhi na mapema muondoke.” Nao wakasema, “Hapana, usiku tutalala mjini.”
3
Lakini akawasihi sana, mwishowe wakaondoka pamoja naye, na wakaingia katika nyumba yake. Akaandaa chakula na kuoka mkate usiotiwa chachu, wakala.
4
Lakini kabla hawaja lala, wanaume wa mji wa Sodoma, vijana kwa wazee wakaizunguka nyumba, wanaume wote kutoka kila kona ya mji.
5
Wakamwita Lutu, na kumwambia, “Wale wanaume walioingia kwako usiku wako wapi? Watoe hapa nje waje kwetu, ili tuweze kulala nao.”
6
Lutu akatoka nje na akafunga mlango.
7
Akasema, “Nawasihi, ndugu zangu, msitende uovu.
8
Tazama, nina mabinti wawili ambao hawajawahi kulala na mwanaume yeyote. Nawaomba tafadhali niwalete kwenu, na muwafanyie lolote muonalo kuwa jema machoni penu. Msitende lolote kwa wanaume hawa, kwa kuwa wamekuja chini ya kivuli cha dari yangu.”
9
Wakasema, “Ondoka hapa!” Wakasema pia, “Huyu alikuja kukaa hapa kama mgeni, na sasa amekuwa mwamuzi! Sasa tutakushugulilia vibaya wewe kuliko wao.” Wakamsonga sana huyo Lutu, na wakakaribia kuvunja mlango.
10
Lakini wale wanaume wakamkamata Lutu na kumweka ndani na wakafunga mlango.
11
Kisha wale wageni wa Lutu wakawapiga kwa upofu wale wanaume waliokuwa nje ya nyumba, vijana na wazee kwa pamoja, kiasi kwamba wakachoka wakati wakiutafuta mlango.
12
Basi wale watu wakamwambia Lutu, “Je una mtu mwingine yeyote hapa? Wakwe zako, wanao na mabinti zako, na yeyote mwingine katika huu mji, ukawatoe hapa.
13
Kwa kuwa tunakaribia kuiangamiza sehemu hii, kwa sababu mashitaka dhidi yake mbele ya Yahwe yamezidi kiasi kwamba ametutuma kuuangamiza.”
14
Lutu akatoka na akazungumza na wakwe zake, wanaume ambao walikuwa wamewaposa binti zake, akawambia, “Ondokeni upesi mahali hapa, kwa kuwa Yahwe anakaribia kuuangamiza mji.” Lakini kwa wakwe zake alionekana kuwa anawatania.
15
Alfajiri, malaika wakamsihi Lutu, wakisema, “Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili ambao wako hapa, ili kwamba usipotelee katika adhabu ya mji huu.”
16
Lakini akakawia-kawia. Kwa hiyo watu wale wakamshika mkono wake, na mkono wa mkewe, na mikono ya binti zake wawili, kwa sababu Yahwe alimhurumia. Wakawatoa nje, na kuwaweka nje ya mji.
17
Wakisha kuwatoa nje mmoja wa wale watu akasema, “Jiponye nafsi yako! Usitazame nyuma, au usikae mahali popote kwenye hili bonde. Toroka uende milimani ili kwamba usije ukatoweshwa mbali.”
18
Lutu akawambia, “Hapana, tafadhali bwana zangu!
19
Mtumishi wenu amepata kibali machoni pako, na umenionyesha wema ulio mkuu kwa kuokoa maisha yangu, lakini sitaweza kutorokea milimani, kwa sababu mabaya yataniwahi na nitakufa.
20
Tazama, ule mji pale uko karibu nijisalimishe pale, na ni mdogo. Tafadhali niacheni nikimbilie pale (Je, siyo mdogo ule?), Na maisha yangu yataokolewa.”
21
Akamwambia, “Sawa, nimekubali ombi hili pia, kwamba sitaangamiza mji ambao umeutaja.
22
Harakisha! Toroka uende pale, kwa kuwa sitafanya chochote mpaka ufike pale.” Kwa hiyo mji ule ukaitwa Soari.