1
Kisha Sarai mke wa Abram, alikuwa hajamzalia mtoto, lakini alikuwa na mtumishi wa kike, Mmisri ambaye jina lake aliitwa Hajiri.
2
Kwa hiyo Sarai akamwambia Abram, “Tazama, Yahwe hajanifanya mimi kuwa na watoto. Nenda na ulale na mtumishi wangu. Ili kwamba niweze kupata watoto kupitia yeye.” Abram akasikiliza sauti ya Sarai.
3
Ilikuwa baada ya Abram kuishi miaka kumi katika nchi ya Kanaani ndipo Sarai, mke wa Abram, alimtoa Hajiri yule mmisri mtumishi wake kwa mume wake awe kama mke wake.
4
Kwa hiyo akawa na mahusiano na Hajiri, na akabeba mimba. Na alipoona kuwa amebeba mimba, akamdharau bibi yake.
5
Kisha Sarai akamwambia Abram, “Jambo hili baya kwangu ni kwa sababu yako. Nilimtoa mtumishi wangu wa kike katika kumbatio lako. Na alipoona kuwa amebeba mimba, nilidharaulika machoni pake. Na sasa acha Yahwe aamue kati yangu na wewe.”
6
Lakini Abram akamwambia Sarai, “Tazama, hapa, mtumishi wako yuko katika uwezo wako, fanya unachofikiri ni kizuri sana kwake.” Kwa hiyo Sarai akakabiliana naye kwa ukatili, na akatoroka.
7
Malaika wa Yahwe akamkuta karibu na chemichemi ya maji katika jangwa, chemichemi iliyo katika njia kuelekea Shuri.
8
Akasema, “Hajiri, mtumishi wa Sarai, umetoka wapi na unakwenda wapi?” Na akasema, “Ninamtoroka bibi yangu Sarai.”
9
Malaika wa Yahwe akamwambia, “Rudi kwa bibi yako, na unyenyekee chini ya mamlaka yake.”
10
Kisha Malaika wa Yahwe akamwambia, “Nitazidisha uzao wako maradufu, kiasi kwamba watakuwa wengi wasioweza kuhesabika.”
11
Malaika wa Yahwe pia akamwambia, “Tazama, wewe unamimba, na utazaa mtoto wa kiume, na utamwita jina lake Ishmaeli, kwa sababu Yahwe amesikia mateso yako.
12
Atakuwa punda mwitu wa mtu. Atakuwa adui dhidi ya kila mtu, na kila mtu atakuwa adui yake, na ataishi kando na ndugu zake wote.”
13
Kisha akamwita jina hili Yahwe aliye zungumza naye, “Wewe ni Mungu unionaye mimi,” kwa kuwa alisema, “Je ninaendelea kweli kuona, hata baada ya kuwa ameniona?”
14
Kwa hiyo kisima kiliitwa Beer Lahai Roi; Tazama, kiko kati ya Kadeshi na Beredi.